Wanawake wawezeshwe kiuchumi kuweka uwanja sawa wa kisiasa

Dar es Salaam. “Tangu nikiwa shule ya msingi, nilikuwa na ndoto ya kuwa kiongozi. Mnamo mwaka 2019, nilifanya ndoto hiyo kuwa kweli kwa kujitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Chakula Bora, Manzese, Dar es Salaam.”

“Safari hii ya uongozi haikuwa rahisi wala ya ghafla; nafasi mbalimbali za uongozi nilizoshikilia tangu shule ya msingi hadi zile za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ngazi ya kata zilinilea na kunijenga kuwa kiongozi imara, mwenye uwezo wa kuhimili changamoto za uongozi.”

Akiwa kwenye mahojiano na Mwananchi yenye lengo la kuangalia changamoto wanazopitia wanawake kwenye uongozi na hatua walichukua baadhi yao kujipambanua na kufanikiwa kuongoza, Oddo Ramadhani, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Chakula Bora, Manzese anasema: “Lazima uwe na ngozi ngumu ili usonge mbele, kwani jamii bado haiamini katika mwanamke, watu wanachokizungumza sicho wanachokiishi kuhusu jinsia yetu,”.

Oddo anasimulia baadhi ya changamoto alizokutana nazo tangu alipojitosha kuwania nafasi hiyo  katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019.

Anasema  alijitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Chakula Bora, ambapo kati ya wagombea 10 walioshiriki katika kinyang’anyiro hicho, alikuwa mwanamke peke yake, lakini alidhamiria kushinda.

“Kutokana na kuwa mgombea pekee mwanamke baadhi ya watu walinibeza kuwa siwezi kuchaguliwa kuhudumu kwenye nafasi hiyo, wengine walidiriki hata kusema hawawezi kuongozwa na mtu anayevaa dera wala kijora,” anaeleza.

Anasema japokuwa maneno yalikuwa mengi lakini hayakumkatisha tamaa ya dhamira yake aliendelea kufanya kampeni zake hadi akafanikiwa kuchaguliwa kuhudumu kwenye mtaa huo.

Anaeleza kuwa hata baada ya kuchaguliwa bado baadhi ya watu waliendelea kutoa maneno ya kebehi ili kumvunja moyo.

“Baadhi ya watu walikuwa wanasema tangu lini mvaa madera na vijora atakuwa kiongozi sitoongoza hata kwa miezi sita, niliziba masikio nikaendelea kuwatumikia wananchi wa mtaa wa Chakula Bora, nashukuru Mungu nimefikisha miaka mitano sasa katika uongozi wangu,” anasema Oddo.

Anasema alitumia kipindi chote cha miaka mitano kuhakikisha anafanya majukumu yake kwa bidii ili kuwathibitishia kuwa mwanamke akipewa nafasi anaweza kuongoza vizuri, huku akiendelea kutekeleza majukumu yake ya familia kama mama na mke.

Alichokisimulia Oddo kinaendana na kile alichokipitia Tatu Kasenene ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa uliopo Magomeni Kagera jijini Dar es Salaam.

Nafasi hiyo aliipata baada ya kukaimishwa majukumu hayo kutokana na aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa kuugua na baadaye kufariki dunia mwaka 2022.

Anasema baadhi ya watu walisema kuwa hawako tayari kuongozwa naye kwa sababu ya jinsia yake.

“Maneno yalikuwa mengi kwa sababu mimi ni mwanamke lakini nashukuru Mungu nimefanikiwa kwa kipindi kilichobaki kutekeleza majukumu ambayo nilikaimu kwa mtangulizi wangu,” anasema.

Dhana ya baadhi ya watu katika jamii kuona mwanamke hawezi kuongoza iliibuliwa pia katika uzinduzi wa mradi wa ‘Wanawake Sasa’ unaolenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Pia kubadili mitazamo kuhusu nafasi na uwezo wa mwanaume na mwanamke katika  uongozi uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Ilibainishwa kuwa moja kati ya changamoto inayorudisha nyumba jitihada za kuleta usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa ni wanawake kuonekana ni watu wasioweza kuongoza.

Changamoto nyingine pia zilizobainishwa ni pamoja na rushwa, uwezo wa kiuchumi pamoja na kukosa ushirikiano kutoka katika ngazi ya familia.

Akizungumzia athari ya changamoto hizo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Taifa (UWT) katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mwajabu Mbwambo amesema zinarudisha nyuma hamasa ya wanawake kushiriki katika masuala ya siasa.

“Wanawake wanaweza kujihisi kuwa siyo jukumu lao kuongoza, au kuhofia kukataliwa na jamii zao na hiyo inatokana na elimu ndogo na uelewa mdogo wa haki zao,”anasema.

Nini kifanyike kuondoa changamoto hizo

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto Zanzibar, Siti Ali alisema pamoja na kumuhamasisha mwanamke kushiriki katika nafasi mbalimbali ni muhimu kwanza kuhakikisha anawezeshwa kiuchumi pamoja na kujengewa uwezo wa uongozi, ikiwemo kuzungumza mbele za watu.

Alisema changamoto ya rasilimali fedha ni moja ya sababu zinazowakwamisha kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi mbalimbali.

“Changamoto ya kiuchumi kuwafanya wanawake washindwe kugharamia kampeni za kisiasa au kushiriki kikamilifu katika uchaguzi,” alisema.

Alishauri wanawake kuendelea kuwezeshwa kiuchumi kwa kupewa mikopo isiyo na riba ili kunapokuwa na chaguzi mbalimbali kuwe na uwanja sawa kati yao na wanaume, kwani ni ukweli kuwa walio wengi wanajiweza kiuchumi.

Kwa upande wake Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Tehama kutoka ACT-Wazalendo,  Rahma Mwita alisema wanawake wanapaswa kuhamasishwa kushiriki kuwania nafasi za uongozi.

“Hata wakiwezeshwa kiuchumi, wakipewa elimu ya ushiriki kwenye hizi chaguzi kusipokuwa na hamasa wanaweza wasijitokeze pia,”alisema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine iendelee kutoa elimu kwa jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa usawa wa kijinsia katika masuala mbalimbali ikiwemo uongozi.  Kuwaelimisha kuwa mwanamke akipewa nafasi anaweza kuongoza vizuri.

Pia alihimiza wanajamii kuachana na dhana potofu kuwa uwepo wa usawa wa kijinsia katika masuala mbalimbali ikiwemo uongozi ni moja kati ya sababu inayoteteresha taasisi ya ndoa.

Gwajima alisema uwezeshwaji wa wanawake kufikia usawa wa kijinsia si sababu ya ndoa kuvunjika kama baadhi ya watu wanavyodhani.

“Nimekuwa nikisikia mahala kila wakitaja masuala ya usawa wa kijinsia minong’ono inaibuka kuwa ‘ndio wanataka kuja kubomoa ndoa eeh’ “

“Nilimsikia mama Mongela akisema ndoa ni taasisi kongwe na kipekee ambayo kanuni zake za uendeshaji haziingiliani na mambo mengine,” alisema.

Alisema ndoa ni mamlaka nyingine yenye utawala wake ambayo ni lazima kuitii na kuiheshimu.

“Ukienda kuibomoa ndoa kwa kuwa umepewa nafasi ya kuwa kiongozi na kuwezeshwa ni kwa utashi wako na wala siyo lengo la kupigania usawa wa kijinsia,” alisema waziri huyo.

Alisema lengo ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na siyo kuwakandamiza wanaume.

Related Posts