Bibi wa miaka 74 auawa kwa kukatwakatwa mapanga

Buchosa. Sarah Petro (74), mkazi wa Kijiji cha Magulukwenda, Kitongoji cha Mizorozoro Kata ya Kalebezo wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza, ameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Mauaji hayo yametokea jana Jumapili Septemba 22, 2024 saa mbili usiku wakati akitokea kwa mtoto wake anayeishi jirani naye.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 23, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amesema vyombo vya dola viko eneo la tukio na vimeanza uchunguzi kubaini waliohusika na mauaji hayo.

“Ni kweli nimepata taarifa ya tukio hilo la kusikitisha na hadi sasa chanzo chake hakijafahamika, vyombo vya dola vinachunguza,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Ngaga amewataka wananchi kuwabaini watu wanaofanya vitendo vya kinyama na kuahidi watu wote waliotenda kosa hilo watakamatwa.

Mtoto asimulia shangazi yake alivyouawa

Naomi Ishengoma, akimzungumzia marehemu shangazi yake, amesema wauaji ambao bado hawajulikani walimvamia wakati akitoka kumsalimia mwanaye saa mbili usiku.

“Wakati shangazi anashambuliwa mimi na mdogo wangu tulikuwa jikoni, alikuwa karibu kabisa na nyumba tulisikia kelele zake, tulipotoka tukamuona mtu aliyekuwa akimkata mapanga amevaa shuka la kimasai, ila alikimbia hatukona alipokimbilia,” amesimulia Naomi.

Naomi ameiomba Serikali kuwasaka na kuwakamata wahusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Petro Paul, mtoto wa marehemu anayeishi Kijiji cha Nyehunge, amesema mama yake hakuwa na ugomvi na mtu yeyote kijijini na ameshangazwa na tukio hilo. Ameitaka Serikali kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.

Mkazi wa Kijiji cha Magulukenda, Bajala Shabani amesema kitongoji chao kimekuwa na matukio ya watu kuvamiwa na kukatwa mapanga mara kwa mara.

Hivyo, ameiomba Serikali kuweka kambi eneo hilo, ili kuwabaini wahalifu wanaofanya vitendo hivyo.

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo aliyefika kutoa pole kwa familia iliyopata msiba huo, amesema vyombo vya dola tayari vinafanya kazi yao na waliohusika na mauaji hayo watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Related Posts