Dar es Salaam. Saa chache baada ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuweka wazi kuwa limewakamata wanachama 14 wa Chadema, wakiwemo viongozi watatu wa chama hicho, Chama cha ACT Wazalendo kimelaani hatua hiyo na kutaka wote waachiliwe huru bila masharti.
Viongozi na wanachama wa Chadema wamekamatwa leo Jumatatu, Septemba 23, 2024 maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kile kilichoelezwa na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro kukaidi amri ya kutoshiriki maandamano.
Maandamano ya maombolezo na amani, yaliitishwa na Chadema na kupanwga kufanyika leo Jumatatu jijini Dar es Salaam, huku kikitaka wanachama na viongozi wa mikoani kufika jijini humo kushiriki maandamano hayo.
Chadema kiliitisha maandamano hayo kupinga matukio ya utekaji na mauaji ya wanachama wake, likiwemo la Ali Kibao lililotokea Septemba 6, 2024 kwa kutekwa akiwa ndani ya basi, eneo la Tegeta na siku moja baadaye mwili wake kuokotwa Ununio.
Kamanda Muliro akizungumza na waandishi mapema leo amesema miongoni mwa hao 14 wanaoendelea kushikiliwa ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Makamu wake-Bara, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.
Wakati Polisi akieleza kuwashikilia 14, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ametoa taarifa kwa umma akidai ni ya awali kuwa viongozi mbalimbali wa majimbo, kanda na wanachama zaidi ya 40 wamekamatwa.
Kutokana na hilo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu ametoa taarifa kwa umma kulaani ukamatwaji huo na kutaka wote waliokamatwa kuachiwa huru bila masharti kwa sababu maandamano ni haki ya kikatiba.
“Tunalaani kwa nguvu zote hatua ya Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi waandamizi wa Chadema na wanachama waliokuwa wanajiandaa kutekeleza haki yao ya kuandamana.
“Pia, tunarejea wito wetu tulioutoa Septemba 22, 2024 kuwa Serikali ichukue hatua za dharura za kuanzisha mazungumzo ya kina na ya dhati yatakayoihusisha Serikali yenyewe, vyama vya siasa, Jeshi la Polisi, viongozi wa dini na wadau wengine wa demokrasia,” amesema Semu na kuongeza;
“Lengo la mazungumzo hayo ni kupata ufumbuzi na kukomesha matukio ya utekaji na mauaji ya raia ambayo ndio yalisababisha kuitishwa maandamano ya leo na pia kushughulikia mambo mengine yanayolalamikiwa yanayohusu demokrasia na haki za binadamu nchini,” amesema Semu.
Katika taarifa hiyo, Semu ameeleza jitihada zinazofanywa na chama chake za kuwafikia viongozi wa Jeshi la Polisi, Chadema, CCM na Serikali kwa ujumla wake kuhakikisha hali inayoendelea inapatiwa ufumbuzi kwa hekima, haki na kwa kutanguliza maslahi mapana ya Taifa.