Dar es Salaam. Maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, yamesimamisha usikilizwaji wa kesi za jinai, na kukwamisha dhamana ya meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob maarufu Boni Yai.
Kutokana na tangazo la Chadema kufanya maandamano leo jijini Dar es Salaam, mahabusu wanaokabiliwa na kesi za jinai katika Mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam, akiwemo Jacob hawakufikishwa mahakamani kusikiliza kesi zao.
Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uongo kwenye mitandao.
Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu Alhamisi Septemba 19, 2024, akasomewa mashtaka mawili, ambayo hata hivyo aliyakana. Upande wa mashtaka uliiomba Mahakama izuie dhamana yake kwa sababu za usalama.
Baada ya mvutano mkali wa hoja za kisheria kuhusiana na uhalali wa maombi hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo aliahirisha mpaka leo Jumatatu, Septemba 23, 2024 saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya uamuzi.
Hata hivyo, leo Boni Yai ambaye yuko mahabusu katika gereza la Segerea, hakufikishwa mahakamani pamoja na mahabusu wengine wanaokabiliwa na kesi tofauti mahakamani hapo.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama hiyo imeshindwa kutoa uamuzi wa pingamizi la dhamana yake pamoja na amri nyingine iliyoombwa na upande wa mashtaka.
Hivyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo ameahirisha uamuzi huo mpaka Alhamisi Septemba 26, 2024.
Wakizungumza na Mwananchi mawakili wa pande zote, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga na kiongozi wa Jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala wamesema Boni Yai hakufikishwa mahakamani kwa sababu za kiusalama, kulingana na hali iliyopo leo.
“Uamuzi umeahirishwa mpaka Septemba 26, 2024 kwa sababu mshtakiwa hajaletwa leo, kutokana na hali ilivyo leo,” amesema Wakili Katuga.
Wakili Kibatala amedai Jacob hakuletwa mahakamani na kwamba kwa taarifa walizonazo na mahabusu wengine Mkoa wa Dar es Salaam hawakufikishwa mahakamani kwa sababu za kiusalama.
“Whether (kama) sababu za kiusalama zipo au hazipo hiyo ni discussion (mjadala) ya siku nyingine. Lakini cha msingi ni kwamba sisi tumeiomba mahakama isome uamuzi halafu utekelezaji kutegemea na maamuzi yatakavyokuwa utafuata baadaye,” amedai Kibatala na kuongeza:
“Lakini Mahakama kwa busara imesema kwa kuwa ni masuala ya dhamana haitakuwa na tija sana kutoa uamuzi wakati mhusika mwenyewe hayupo. Kwa hiyo tumeahirisha mpaka Alhamis Septemba 26, 2024, saa 5 asubuhi ambapo sasa tutafahamu hatima ya dhamana na hayo maombi mengine,” amesema.
Hata hivyo, wakati Boni Yai akikwama mahabusu, mmoja wa wadhamini wake waliokuwa wameandaliwa leo, Emmanuel Ntobi ametiwa mbaroni nje ya geti la Mahakama ya Kisutu.
Wakili Kibatala amedai Ntobi alikuwa ni miongoni mwa wadhamini wa Boni Yai na kwamba alifika mahakamani hapo kwa lengo hilo.
Hata hivyo, amedai alipofika kwenye lango kuu la kuingilia mahakamani hapo, baada ya kuhojiwa na askari Polisi waliokuwa wametanda langoni hapo akajieleza kuwa anakwenda kwenye kesi ya Jacob kama mdhamini hapohapo amekamatwa na kupelekwa katika kituo cha Polisi Oysterbay.
Hata hivyo, si Boni Yai pekee ambaye hajafikishwa mahakamani, bali mahabusu wote wanaokabiliwa na kesi mahakamani hapo Kisutu.
Mbali na Kisutu habari kutoka Mahakama Kuu Dar es Salaam pia zilieleza hakuna gari la mahabusu lililowapeleka mahabusu mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi zao.
Mashtaka hayo ni kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.
Alisomewa mashtaka hayo na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, Nurati Manja.
Katika shtaka la kwanza Wakili Manja alidai kuwa, Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).
Tofauti na siku nyingine hali ya usalama keo katika Mahakama ya Kisutu iliimarishwa na askari wengi wa Jeshi la Polisi waliokuwa na sare pamoja na silaha na walikuwa wamevaa kiraia, waliokuwa katika Kona mbalimbali za mahakama hiyo.
Katika lango la kuingilia mahakamani hapo kulikuwa na ukaguzi wa hali ya juu magari na kila aliyetaka kuingia hapo huku kila mmoja akihojiwa sababu iliyokuwa inampeleka hapo.
Wale waliodai wanakwenda kwenye kesi walitakiwa kutaja ni kesi gani iko kwa hakimu gani pamoja na uhusika wao katika kesi husika na wale walioshindwa kujieleza na au hawakuwa na sababu za msingi wakizuiliwa kuingia.
Hivyo watu wengi waliofika mahakamano hapo kwa ajili ya kufuatilia kesi ya Boni Yai wakiwemo ndugu jamaa marafiki na hata wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema wakijikuta wakizuiliwa kuingia.
Hali hiyo haikuishia kwa wananchi wa kawaida bali hata mawakili wa kujitegemea ambao ni maafisa wa Mahakama walijikuta katika adha hiyo ya kuhojiwa na kupekuliwa kwa kina na hata kurushina maneno baina ya askari Polisi hao na baadhi ya mawakili.
Kutoka na udhibiti huo wa watu walioingia mahakamani hapo, tofauti na siku nyingine ambazo mahakama hiyo huwa na watu wengi wanaongia na kutoka, leo kulikuwa na watu wachache sana, huku kukiwa na utulivu mkubwa.
Mbali na watumishi, wengi walioruhusiwa kuingia mahakamani hapo ni mawakili wa Serikali na wa kujitegemea pamoja na wananchi wachache wenye kesi na waliojieleza vema kwa askari.
Hali hiyo ya ulinzi na ukaguzi iliendelea mpaka saa Saba mchana muda mfupi tu bada ya mawakili wa Jacob, Kibatala na wenzake, Michael Lugina, Dickson Matata, Deogratias Mahinyila kuondoka mahakamani hapo, ndipo askari polisi hao pia walipoondoka.