YANGA Princess katika kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao imemshusha mshambuliaji kutoka CBE ya Ethiopia, Aregash Kalsa.
Huyo anakuwa mchezaji wa pili kutoka Ethiopia kusajiliwa na Yanga Princess msimu huu baada ya siku chache zilizopita kumtambulisha Arieth Udong.
Hadi sasa mshambuliaji huyo bado hajatambulishwa rasmi kikosini hapo lakini wiki ya pili sasa anafanya mazoezi na wenzake kujiandaa na michezo ya Ngao ya Jamii itakayochezwa Oktoba 2 mwaka huu sambamba na mechi za ligi.
Mwanaspoti lilimshuhudia nyota huyo kambini akiwa na wenzake huku pia akijumuishwa kwenye program za timu.
Mratibu wa Yanga Princess, Kibwana Matokeo, alipotafutwa kwa ajili ya kumzungumzia mshambuliaji huyo na kikosi kwa ujumla, alisema: “Bado hatujamaliza kutambulisha wachezaji, kuna wengine watashushwa, kaeni tayari.”
Licha ya hayo yote lakini chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kililiambia Mwanaspoti kuwa kuchelewa kutambulishwa kwa mchezaji huyo kulitokana na ishu za Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ambapo hivi tayari mambo yapo sawa baada ya awali kukwama.
“Nafikiri suala lilikuwa ITC ndio changamoto kubwa na shida ilikuwa kwao Ethiopia walichelewa kutoa lakini hadi sasa mambo yako sawa, kilichobaki ni wenyewe Yanga kumtambulisha,” kilisema chanzo hiko.
Kalsa msimu uliopita akiwa na C.B.E alicheza mechi 11 kwa dakika 990 na kufunga mabao 16 akiwa hana asisti.