BAADA ya kutupia bao moja na kutoa pasi mbili za mwisho zilizozaa mabao mawili kati ya sita yaliyofungwa na Yanga Jumamosi iliyopita, kiungo wa timu hiyo, Mudathir Yahya ameonekana kuridhishwa na rekodi anazoendelea kuziweka kikosini hapo.
Kiungo huyo ambaye alijiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2022-2023, Jumamosi iliyopita alikuwa sehemu ya kuchangia kikosi cha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika waliposhinda 6-0 dhidi ya CBE SA. Ukiondoa bao moja la Mudathir, wafungaji wengine ni Clatous Chama, Clement Mzize, Duke Abuya na Stephane Aziz Ki aliyefunga mawili.
Yanga kuingia makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ni rekodi nyingine kwao ikiwa wamefanya hivyo mara mbili mfululizo kwa mara ya kwanza, huku pia ikifunga mabao 17 katika mechi nne bila ya kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mudathir alisema anajivunia kuwa sehemu ya wachezaji wa Yanga waliotumika kwa kiasi kikubwa kutoa mchango wa kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili mfululizo.
“Nimefunga na kutoa asisti mbili, nina furaha na najiona nakua kiuchezaji, ukiondoa imani kubwa iliyopo kwa wachezaji wazawa chini ya makocha wote wawili ambao wameipa Yanga mafanikio kimataifa, Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi, kiwango changu kinaongezeka na mafanikio ya timu pia yanasogea,” alisema na kuongeza:
“Ubora wa mchezaji mmojammoja ndani ya kikosi cha Yanga umekua chachu kubwa ya mimi kujiweka kwenye ushindani kwa sababu nikiamini kuwa nipo fiti na nina uhakika wa namba, hivyo juhudi na maarifa naviongeza kwenye kila mchezo pale ninapopata nafasi ya kucheza.”
AFICHUA NOTI ZILIVYOWAPA MZUKA
Wakati ikifahamika kwamba Yanga wamelamba shilingi milioni 30 kutokana na kufunga mabao sita katika mchezo huo ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya Goli la Mama, Mudathir amefichua siri ya nyota hao kucheza kwa ubora zaidi na kukimbiza mpira kati kila wanapopachika bao.
Kiungo huyo alisema mbali na ahadi ya Goli la Mama, pia mdhamini na mwekezaji wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ aliwaahidi Sh5 milioni kwa kila bao.
“Ubora mkubwa ulioonyeshwa na kikosi chetu ni kutokana na ahadi kutoka kwa Rais wa nchi na mdhamini wetu ambaye pia aliweka ahadi, hiyo ndiyo ilileta mzuka ndiyo maana ulikuwa unaona kila tukipachika bao tunakimbilia kuweka mpira kati ili tuanzishe haraka,” alisema.