TMDA yaonya wanaosafirisha dawa za binadamu kwa matenga

Mtwara. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kusini imekamata dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh200,000 wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara zilizokuwa zikisafirishwa kwa pikipiki ndani ya matenga, kinyume cha sheria.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 23, 2024 baada ya kumkamata mkazi wa Masasi aliyekuwa akisafirisha dawa hizo, Mkaguzi wa TMDA Kanda ya Kusini, Horrace Mbungani amesema aina hiyo ya usafirishaji inasababisha dawa kupoteza ubora na kuzifanya ziwe na usugu wa vimelea kwa watumiaji.

Mbungani amesema usafirishaji holela wa dawa, hususan zile zinazoharibika kwa urahisi zinapopigwa na jua, ni mojawapo ya sababu zinazochangia dawa kupoteza ufanisi wake. Ameongeza kuwa dawa nyingi zinahitaji kuhifadhiwa katika mazingira maalumu, ili ziendelee kuwa na ubora wa kutibu magonjwa.

“Fikiria mtu akisafirisha dawa kwenye pikipiki, zikiwa kwenye matenga, muda wote wa safari zinapigwa na jua, hivyo kupoteza ubora wake. Hapo, badala ya kupata tiba sahihi, watumiaji wanakula dawa zisizokuwa na nguvu za kutibu magonjwa,” amesema Mbungani.

Aidha, amesema TMDA imebaini ongezeko la bodaboda zinazobeba bidhaa mbalimbali, ikiwemo dawa, kwa njia zisizokubalika.

Mbugani amesema hali hiyo inahatarisha usalama wa dawa kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Hivyo, ametoa wito kwa jamii kuacha mara moja kusambaza dawa kwa njia hizo.

Mbungani pia amesema baadhi ya watu wanaosafirisha na kuuza dawa hawana ujuzi wala vibali vya kufanya hivyo, jambo alilosema linachangia kuongeza hatari zaidi.

Anthony John, mkazi wa Ndanda, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti uuzaji wa dawa mitaani, ili kulinda afya za watumiaji. Amesema kununua dawa kwenye maduka yasiyo rasmi kunasababisha madhara makubwa, ikiwemo usugu wa vimelea mwilini bila watumiaji kufahamu.

Related Posts