KOCHA wa zamani wa Yanga, Milutin ‘Micho’ Sredojevic, ameipongeza Simba kwa kiwango kizuri ilichokionyesha katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli huku akibainisha kwamba inaweza kucheza na mpinzani yeyote na kufanya vizuri.
Micho ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Simba kuichapa Al Ahli Tripoli mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mabao 3-1.
Mserbia huyo aliushuhudia mchezo huo akiwa uwanjani ambapo alikuja kwa lengo la kuiongezea nguvu Al Ahli Tripoli ambapo moja kwa moja alionyesha kukubali kiwango cha Simba. “Simba walicheza kwa ustadi mkubwa na walitumia vyema nafasi zao, kwa hakika walistahili ushindi huo,” alisema kocha huyo aliyewahi kuinoa Yanga 2007.
“Simba wanaonyesha wapo katika mwendelezo mzuri. Ushindi huu unaonyesha wana uwezo wa kupambana na timu yoyote barani Afrika.”
Hata hivyo, Micho alitoa pongezi kwa jitihada zilizofanywa na benchi la ufundi la Al Ahli Tripoli, akisema walijaribu kwa uwezo wao lakini walikumbana na timu yenye ubora.
Aliongeza kuwa anakumbuka alipokuwa kocha wa Yanga, na hivyo anafahamu soka la Tanzania lilivyoendelea kwa kasi.
Katika hatua nyingine, Micho alimpongeza Kocha wa Simba, Fadlu Davids, ambaye aliwahi kuwa msaidizi wake alipokuwa Orlando Pirates kwa kuipeleka Simba hatua ya makundi.
Katika maelezo yake, Micho alisisitiza kuwa Simba wamepiga hatua kubwa katika soka la Afrika na ni wazi kwamba juhudi za benchi la ufundi na wachezaji zinalipa.
Kocha huyo pia alitoa wito kwa timu za Afrika kuendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kama Kombe la Shirikisho, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yana umuhimu mkubwa kwa ukuaji wa soka la bara hili.
“Haya mashindano ni muhimu sana kwa timu za Afrika yanafungua milango kwa wachezaji wetu na kuinua hadhi ya ligi zetu,” alisema Micho.
Akizungumzia maendeleo ya soka Tanzania, Micho alisema Simba na Yanga zimekuwa timu za mfano katika kuendeleza vipaji huku akimalizia kwa kuzitakia kila la heri katika hatua ya makundi, akiamini kuwa siku moja wanaweza kuleta mataji nyumbani.
Ikumbukwe kwamba, Simba imefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati Yanga ikitinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo sasa zinasubiri droo ya upangaji wa ratiba ya hatua hiyo itakayofanyika Oktoba 7 mwaka huu.