Dar es Salaam. Ni hekaheka. Ndivyo unaweza kusimulia hali ilivyokuwa katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia asubuhi hadi jioni.
Askari wa Jeshi la Polisi walitanda maeneo mbalimbali kuhakikisha hali ni shwari.
Ulinzi huo ulitawala hasa maeneo ya makutano ya barabara mathalani Ubungo, Mwenge, Tazara, Buguruni, Kilwa na maeneo ya Kariakoo na Mnazi Mmoja, kuhakikisha hakuna mtu anayeandamana.
Magari yenye askari yalirandaranda huku na huko huku wengine wakiwa wamesimama katika makutano hayo wakiwa na silaha.
Askari wenye silaha za moto na wengine wenye virungu na vifaa vya kujikinga, walionekana wakizunguka katika mitaa mbalimbali ya jiji, huku magari maarufu ya ‘washawasha’ na mengineo kama ‘defeder’ yakiwa yameegeshwa kwenye makutano ya barabara.
Msingi wa yote ni kuhakikisha wanadhibiti vilivyo maandamano yaliyoitishwa Septemba 11, 2024 na Chadema, waliyoyaita ya maombolezo na amani. Chama hicho kilisema kinapinga matukio ya utekaji na mauaji dhidi ya wanachama wake na wananchi wengine.
Kamati Kuu iliyoketi siku hiyo ilitoa tangazo hilo la maandamano kufanyika Dar es Salaam na kuwataka wanachama, viongozi wa mikoani kufika jijini humo kushiriki maandamano hayo yaliyokuwa na njia mbili. Ilala Boma hadi Mnazi Mmoja na nyingine Magomeni hadi Mnazi Mmoja.
Tukio la karibuni la utekwaji wa wananchi, ni la Septemba 6, 2024 wakati mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao alipotekwa eneo la Kibo Complex, Tegeta, Dar es Salaam akiwa ndani ya basi akisafiri kwenda nyumbani kwake jijini Tanga.
Katikati ya mjadala na kuhoji alipo Kibao, mwili wake uliokotwa eneo la Ununio ukiwa umetupwa. Taarifa ya awali ya uchunguzi wa kitabibu uliofanywa Hospitali ya Rufaa ya Mwanyamala iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ilidai Kibao aliteswa kabla ya umauti na uso wake ulimwagiwa tindikali.
Mbali na tukio hilo la Kibao, Chadema wanaishinikiza Serikali kueleza walipo Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise.
Kiongozi wa Chadema, wilaya ya Sumbawanga, Rukwa, Dioniz Kipanya, naye inadaiwa alitekwa, hajulikani alipo. Chadema walitaka viongozi wenye dhamana ndani ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani wajiuzulu na ndio msingi wa kuitishwa kwa maandamano.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake, David Misime ilipiga marufuku maandamano hayo na kusisitiza atakayekaidi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kuhakikisha maandamano hayafanyiki ulinzi uliimarishwa vilivyo.Ulinzi huo kuna nyakati ulisababisha adha ya shughuli za kijamii kama foleni kutokana na baadhi ya maeneo barabara kutopitika kwa urahisi.
Hata hivyo, maandamano hayo hayakufanyika. Polisi walianza kuimarisha ulinzi tangu juzi na Jumatatu, kuanzia asubuhi uliimarishwa zaidi ikiwemo kwenye makazi ya viongozi wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu wake-Bara, Tundu Lissu.
Mbali ya hao, Dk Lilian Mtei ambaye ni mke wa Mbowe pamoja na binti yao, Nicole walikamatwa na Jeshi la Polisi. Walipelekwa Kituo cha Polisi Osterbay. Baadaye waliachiwa.
Askari wenye silaha walikuwa nje ya makazi ya Mbowe, Mikocheni wakilinda na kila aliyepita maeneo hayo alihojiwa anakwenda wapi. Vivyo hivyo kwa Lissu anayeishi Tegeta. Hata hivyo, Mbowe hakuwapo ndani mwake zaidi ya wanafamilia.
Polisi ilitangaza kuwatia nguvuni watu 14 akiwemo Mbowe, Lissu, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema kutokana na kukaidi amri halali ya kusitisha maandamano hayo.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari, alisema watu hao walikuwa wanaendelea kufanyiwa mahojiano kisha hatua zaidi ziendelee kuchukuliwa dhidi yao.
“Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa 14 ambao wamekiuka tamko la Jeshi la Polisi wakiwa wanaendelea kuyapanga na kutaka kufanya maandamano ambayo yalishapigwa marufuku,” alisema Kamanda Muliro na kusisitiza hali ya jiji hilo ni shwari.
Wakati kamanda Muliro akieleza kushikiliwa kwa viongozi hao watatu na wanachama wengine 11, Chadema ilitoa taarifa yake inayoeleza kuwa wapo viongozi wengine na wanachama zaidi 40 wa kanda ya Pwani waliokamatwa.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema iliwataja viongozi wengine waliokamatwa ni Naibu Katibu Mkuu Bara Benson Kigaila, mwenyekiti wa Mkoa wa Katavi Rhoda Kunchela na Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi.
Wengine waliokamatwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni wanafamilia wa Mbowe ambao ni mkewe Dk Lilian Mtei na mtoto wake Nicole Mbowe pamoja na walinzi na watumishi wa ofisi za chama waliokuwa ofisini.
‘’Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuheshimu haki zote za waliokamatwa na kuwatendea kama watu ambao sio wahalifu kwa wakati wote wa kushikiliwa kwao,” alisema Mrema.
Walivyokamatwa Mbowe, Lissu
Lissu yeye alikamatwa nyumbani kwake Tegeta ambapo magari matatu yenye askari yalifika kwake na kumweleza anahitajika kwa Mkuu wa Polisi wa Upelelezi (RCO) wa Kinondoni. Lissu alitoa taarifa ya uwepo wa polisi kupitia akaunti yake ya kijamii ya X (zamani Twitter).
Mwanasiasa huyo alisema atakwenda. Alichukuliwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Mbweni ambapo hadi jioni ya Jumatatu aliendelea kushikiliwa hapo. Wakili wake, Hekima Mwasipu akizungumza na Mwananchi nje ya kituo hicho alisema, Lissu amehojiwa akituhumiwa kuhamasisha watu kufanya vurugu kupitia maandamano.
“Ametajiwa kosa la kuhamasisha watu kufanya vurugu kupitia maandamano haramu,” alidai Wakili Mwasipu. Alisema baada ya kuandika maelezo amerudishwa mahabusu. “Tunasubiri dhamana.’’ Alisema.
Wakati Lissu akikamatwa nyumbani kwake, Mbowe yeye alijikuta akiingia mikononi mwa Polisi eneo la Magomeni alipotaka kuanza kuandamana kuelekea Mnazi Mmoja. Alifika eneo hilo, saa 4:20 asububi akiwa ameambata na mtoto wake, Nicole.
Baada ya kushuka kwenye gari alianza kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwepo kwenye eneo hilo. Tofauti na ambavyo imezoeleka kwa kiongozi huyo kutumia gari aina ya V8, aliwasili akiwa kwenye gari dogo na hakuwa ameambatana na walinzi wake kama ilivyo kawaida.
Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kushangazwa na nguvu kubwa iliyotumika ikiwemo kuzingirwa kwa nyumba za viongozi wa Chadema ingawa kwa bahati yeye hakuwa nyumbani kwake.
“Bado tunadai kupatikana kwa viongozi wetu, waliotekwa na kupotezwa na bado kuna madai yetu kuhusu matukio ya watu kutekwa na kuauwa. Maandamano ni haki ya kikatiba pale nguvu kubwa inapotumika, kukusanya askari wenye silaha kwa gharama za walipa kodi, siyo sawasawa wala haki.
“Maandamano yetu ni amani na maombelezo ambayo hayakusudii kumdhuru mtu yeyote yule, sasa tunasikitika nguvu kubwa kutumika kutisha raia na kunyima uhuru wao, sasa nimelazimika kuja hapa ambapo ndiyo ilikuwa eneo la kuanzia maandamano ili kuona hali halisi ni nini,” amesema Mbowe.
Wakati bado akiendelea kuzungumza na waandishi, askari walikatisha mazungumzo hayo kwa kumkamata Mbowe na kuondoka naye. Vivyo hivyo kwa Nicole naye alikamatwa eneo hilohilo.
Mwananchi lililokuwa limeweka kambi maeneo mbalimbali, lilishuhudia ukamati wa wafuasi, viongozi na wanachama wa Chadema ukifanyika pasipo kutumia nguvu, kupigwa.
Waliokamatwa walishikwa mikono ama kuelekezwa kwenye magari yaliyokuwa eneo husika na kupanda kisha kupelekwa vituoni kikiwemo Kituo Kikuu cha Polisi, Mbweni, Oysterbay, Buguruni. Taarifa zinaeleza Lema yeye alikamatwa Uwanja wa Ndege, Dar es Salaam alipotua akitokea Arusha.
Wakili Peter Kibatala aliyekuwa na mawakili wengine Kituo cha Osterbay alidai zaidi ya makada na viongozi 30 wa chama hicho, akiwemo Mbowe wanashikiliwa kutuoni hapo.
“Lema yeye yupo kituo cha polisi cha uwanja wa ndege, mimi (Kibatara) nipo hapa Oysterbay naongoza timu ya mawakili wenzangu nane kutoa huduma za kisheria kwa wote waliokamatwa akiwemo Kigaila,” alisema Kibatala na kuongeza:
“Mbowe amefanyiwa mahojiano tayari kwa kosa la kuandamana bila kibali, wote waliokamatwa tutatoa huduma za kisheria kwa kujigawa kulingana na mahitaji.”
Mwananchi ilishuhudia makada na wafuasi wa Chadema waliojitokeza kwa ajili ya kuandamana, wakikamatwa katika eneo la Ilala Boma huku wengine wakishushwa kwenye daladala.
Polisi walionekana kuchunguza kila daladala linaloingia mjini kutokea maeneo ya Kigogo na kuwachomoa wale wanaowatilia shaka kuwa ni waandamanaji na kuwaweka kwenye magari.
Aidha, Polisi katika maeneo mbalimbali walionekana kuwapiga marufuku waandishi wa habari kuonekana maeneo hayo na kuwataka kuondoka hali iliyokuwa ikiibua mvutano baina yao, kwa kile kilichokuwa kikielezwa wanatekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma kinachoendelea.
Eneo la kuzunguka Soko la Kimataifa la Kariakoo, shughuli mbalimbali za kiuchumi ziliendelea huku kukiwa na idadi ndogo ya wateja.
Mmoja wa wafanyabiashara, Juma Othman alilalamikia biashara kudorora kutokana na tishio la uwepo wa maandamano hayo.
“Jumatatu ni siku iliyochangamka hapa Kariakoo kwa kuwa maduka ya jumla huuza kwa wingi bidhaa na wateja wa jumla huwa wanakuwa wengi, leo wamepungua sana hivyo mzunguko wa watu umekua mdogo na mzunguko wa kifedha unapungua pia,” alisema Juma.
“Kwa leo biashara imedorora, ijapokuwa tunauza lakini nahisi wateja wameogopa kuja kuhofia maandamano. Awali polisi walikuwa wakizunguka Kariakoo lakini kwa sasa wameondoka ni wachache tunawaona,” alisema mchuuzi wa vijora aliyejitambulisha kwa jina la Amina Hassan.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na ACT-Wazalendo wamelaani kukamatwa kwa wanachama na viongozi hao na kulitaka Jeshi la Polisi kuwaachia pasipo masharti yoyote.
Taarifa ya LHRC iliyotolewa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Dk Anna Henga imesema maandamano hayo yalikuwa na lengo la kuomboleza na kufikisha ujumbe kuhusu matukio ambayo yamekuwa yakiendelea ya utekaji, ukamataji kiholela na mauaji.
LHRC imetoa wito kwa mamlaka, kutekeleza majukumu yao ya ulinzi wa raia pale wanapotekeleza kwa amani haki zao za kikatiba, kuwaachia mara moja viongozi wa chama cha siasa waliokamatwa bila mashitaka yanayowakabili kuwekwa wazi.
“Kuheshimu misingi ya sheria katika ukamataji wa raia wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai. Kufanya uchunguzi wa matukio ya kupotea, utekaji nyara na mauaji ambayo yamezua hofu kubwa nchini na ndio kilio kikubwa cha waandamanaji,” amesema Dk Henga.
Wito kama huo ulitolewa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu kupitia taarifa kwa umma, akilaani ukamatwaji huo na kutaka wote waliokamatwa kuachiwa huru bila masharti kwa sababu maandamano ni haki ya kikatiba.
“Tunalaani kwa nguvu zote hatua ya Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi waandamizi wa Chadema na wanachama waliokuwa wanajiandaa kutekeleza haki yao ya kuandamana.
“Pia, tunarejea wito wetu tulioutoa Septemba 22, 2024 kuwa Serikali ichukue hatua za dharura za kuanzisha mazungumzo ya kina na ya dhati yatakayoihusisha Serikali yenyewe, vyama vya siasa, Jeshi la Polisi, viongozi wa dini na wadau wengine wa demokrasia,” amesema Semu na kuongeza;
“Lengo la mazungumzo hayo ni kupata ufumbuzi na kukomesha matukio ya utekaji na mauaji ya raia ambayo ndio yalisababisha kuitishwa maandamano na pia kushughulikia mambo mengine yanayolalamikiwa yanayohusu demokrasia na haki za binadamu nchini,” alisema Semu.
Katika taarifa hiyo, Semu alieleza jitihada zinazofanywa na chama chake za kuwafikia viongozi wa Jeshi la Polisi, Chadema, CCM na Serikali kwa ujumla wake, kuhakikisha hali inayoendelea inapatiwa ufumbuzi kwa hekima, haki na kwa kutanguliza maslahi mapana ya Taifa.