Kilwa. Wananchi wa kijiji cha Zinga kilichopo wilayani Kiwa Mkoa wa Lindi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya umeme kwa muda mrefu sasa wamepatiwa ufumbuzi.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 23, 2024, baada ya kuwashwa kwa umeme wa REA kijijini Zinga Kibaoni, Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassani Saidi amesema Mkoa wa Lindi umebakisha vijiji 16 katika Wilaya ya Kilwa ambavyo bado havijaunganishwa na umeme wa REA.
Amesema kukamilika kwa kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji hivyo kunaufanya Mkoa wa Lindi uwe umeunganisha umeme katika vijiji vyote 524 vya mkoa huo.
“Wilaya ya Kilwa imebakisha vijiji 16 ambavyo bado havijaunganishwa na umeme wa REA. Vikikamilika, tutakuwa tumeshakamilisha vijiji 524 kwa Mkoa wa Lindi,” amesema Saidi.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Athumani Jumbe amesema kuwashwa kwa umeme katika kijiji cha Zinga kutaleta chachu ya maendeleo na kuongeza pato la Taifa.
“Umeme ukiwa sehemu yoyote unasaidia wananchi kufanya biashara muda wowote, hivyo kuongeza chachu ya maendeleo na kuchangia pato la wilaya, mkoa, hadi taifa. Tunamshukuru Rais Samia kwa kuhakikisha umeme unafika vijijini,” amesema Jumbe.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Zinga, Ally Ndekule amesema ujio wa umeme utawasaidia wananchi kufanya biashara mbalimbali zinazotegemea umeme, tofauti na awali.
“Kijiji hiki kina wakazi zaidi ya 9,000, lakini hadi sasa ni wakazi 21 tu waliounganishwa na umeme. Naomba wananchi wenzangu wajitokeze kwa wingi kuweka umeme, ili tuwe na maendeleo makubwa zaidi kijijini kwetu,” amesema Ndekule.
Mjasiriamali wa dawa za mifugo, Mercy Njau amesema awali alikuwa akikumbana na changamoto ya kushindwa kuhifadhi dawa kwenye majokofu, lakini sasa ataweza kuzihifadhi na kufanya biashara muda wote.
“Tunashukuru sana Serikali yetu kwa kutujali. Awali nilikuwa napata shida katika biashara, nilikuwa nashindwa kuhifadhi dawa za mifugo kwenye jokofu kwa sababu ya kukosa umeme, na pia nililazimika kufunga maduka mapema. Sasa hivi, nitaweza kuuza hadi usiku,” amesema Njau.
Naye Shija Juma, mfugaji na mfanyabiashara wa nyama ya ng’ombe, amesema umeme utawasaidia kuhifadhi nyama kwenye majokofu wanapochinja, ili isiharibike.
“Kwa kweli wakazi wa Zinga tumeteseka sana kwa muda mrefu kuishi bila umeme. Tulikuwa tunachinja ng’ombe na nyama ikibaki hatukuwa na sehemu salama ya kuhifadhi, tulilazimika kuikopesha ili isiharibike. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea umeme, sasa tutafanya biashara muda wowote,” amesema Juma.
Wakati huohuo, REA imetoa mitungi ya gesi 30 kwa wajasiriamali na wazee, ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.