Polisi wadai mwanafunzi anayedaiwa kupotea mlimani hakufika kwenye kilele

Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Joel Johannes (14), mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara, hakufika kileleni mwa Mlima Kwaraa pamoja na wenzake wakati wa ziara ya masomo iliyofanyika Septemba 14, 2024. Mwanafunzi huyo aliripotiwa kupotea tangu siku hiyo.

Licha ya juhudi za kumtafuta mwanafunzi huyo kwa kutumia ndege isiyo na rubani (drone) katika eneo la mlima huo, bado hazijazaa matunda.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, amesema uchunguzi wa awali umebaini Joel hakufika kwenye kilele cha mlima pamoja na wenzake kama ilivyotarajiwa.

Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta mwanafunzi huyo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini kilichotokea.

“Hatujampata mwanafunzi bado kilichoonekana katika uchunguzi wa awali hakupanda juu ya mlima, tumemtafuta hadi kwa kutumia drone, lakini hatukumpata akiwa hai au akiwa amekufa,” amesema kamanda huyo na kuongeza;

“Baada ya kuchakata taarifa za mwanzo, ikiwemo kwa wenzake, ni wazi hakupanda mlima, licha ya kumtafuta kwa siku kadhaa, tunaendelea kumtafuta nje ya mlima ule ili tujue alipo.”

Mwishoni mwa wiki, baadhi ya wanafunzi wenzake waliokuwa naye siku hiyo walipokwenda katika safari hiyo ya masomo, walidai mwanafunzi huyo hakuwa sawa na alikuwa akijitenga na wenzake.

Kwa mujibu wa mkuu wa shule hiyo, Emanuel Dahaye, katika mazingira ya sasa wanahisi mwanafunzi huyo ametoroka na yuko mtaani, hivyo kwa sasa nguvu kubwa inapelekwa huko kumtafuta.

“Katika mazingira haya tunahisi kijana ametutoroka yuko mtaani, kwa hiyo hatua inayofuata sasa ni kupeleka nguvu kubwa mtaani kumtafuta. Hii ni changamoto katika kazi, tunaomba Mungu tutafanikiwa tunaendelea kumtafuta hatujakata tamaa, tuna imani atapatikana,”alisema mkuu huyo wa shule.

Alisema siku ya safari ya kimasomo, Septemba 14, 2024 ilihusisha wanafunzi wa kidato cha pili waliokuwa 103 ambapo kati yao wasichana walikuwa 62 na wavulana 41 na kuwa baada ya mwanafunzi huyo kupotea walianza kumsaka hadi leo bila mafanikio.

Baadhi ya wanafunzi wenzake walipanda naye mlima walidai siku hiyo mwenzao alikuwa tofauti na siku nyingine na alikuwa na hali ya kujitenga tofauti na ilivyo siku zote.

Mmoja wa wanafunzi hao, Amani Mollel, alidai wakiwa wanapanda kwa makundi, yeye akiwa kundi la pili na wenzake, walipokaribia kileleni walimkuta Joel amekaa chini ya mti peke yake akijikuna kwa madai amepita kwenye majani yamemuwasha.

“Tunakuambia twende, akakataa akasema nyie nendeni mtanikuta hapa nimekaa kwenye kivuli, tukamlazimisha hadi akatukubalia akatufuata tukawa tunatembea naye na baadaye tukakutana na grupu lingine, tukafuata njia moja tukakuta njia imefungwa.

“Tukasema tungalie kama njia ipo na wakati huo Joel tulikuwa naye, ila tulipofika mbele walimu wakatuita tukaanza kugeuka nikamwambia Joel turudi kule akasema sawa, ila alikuwa anaonyesha hana nia ya kurudi, ana mpango wa kuendelea mbele, tukafika mbele tukapotea tena tukakuta njia imefungwa,” alieleza mwanafunzi huyo.

Alidai Joel aliendelea kuwa nyuma na yeye alitangulia mbele kuangalia njia na alipobaini njia hiyo haitoki wakakubaliana kurudi.

“Wakati tunageuza hapo ndipo alipochoropoka hadi tulipokutana na wenzetu tukagundua alikuwa hayupo. Hana tabia hiyo, mimi nahisi kuna kitu, tunahisi Joel ameshuka chini ya mlima yuko mtaani amejificha.

“Anajua anatafutwa na amefanya kosa anaamini akipatikana atapewa adhabu kali, kama ataona hii tunamshauri aangalie wazazi wake wanavyoteseka, arudi tu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Babati, Halfan Matupula alisema licha ya kuongeza nguvu, ikiwemo mgambo 60 walioungana na vyombo vingine vya usalama, wananchi na wazazi tangu siku hiyo hadi sasa hawajafanikiwa kumpata.

“Wametafuta siku hizi zote wakiungana na wazazi na wazazi na timu imejiridhisha mtoto hajapatikana na ni kweli hayupo na kwa mujibu wa mhifadhi kwa maeneo ambayo yanafikika wameyapitiwa,”alisema.

Halfan alisema kwa sasa jitihada zinapelekwa upande mwingine kwa jamii, kwa sababu inawezekana mwanafunzi huyo amepotea kweli baada ya kuachwa na wenzake mlimani akashuka mwenyewe.

“Lakini pia kuachwa na wenzake hilo linaweza kuwa ni kosa sana na anafahamu wazazi wanamtafuta huenda yuko kwa wenzake, amekaa anakuwa na hofu, tunachokifanya sasa hivi ni kupita kwenye maeneo ya karibu,” alisema.

Halfani alisema, “Kwenye nyumba wanazokaa wanafunzi wamepanga, tumeongea na wazazi huenda mtoto amepata hofu kurudi nyumbani, waulize nyumbani kwa ndugu na jamaa. Ila jitihada zimefanyika na kazi inaendelea uchunguzi wa jeshi la polisi unaendelea.”

Related Posts