Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula, amepongeza mchango mkubwa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kukuza utalii ikolojia na kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini.
Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye maeneo yanayosimamiwa na TFS jijini Tanga Septemba 23 2024, Mabula alisisitiza umuhimu wa utalii endelevu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi huku ukiendelea kulinda mazingira.
Mabula alieleza kuwa utalii wa misitu ni moja ya nyenzo muhimu za kuongeza mapato kwa jamii za ndani na wakati huohuo kuhamasisha uwajibikaji miongoni mwa wakazi.
“Utalii ikolojia hauleti tu faida kwa jamii, bali pia unasaidia katika kuwafanya watu wa maeneo haya kutambua umuhimu wa kuhifadhi rasilimali zao za asili,” alibainisha Mabula.
Aliongeza kuwa TFS imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha misitu inatumika kwa njia endelevu ili kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kwa mfano, leo nimetembelea na kujionea misitu ya mikoko, magofu ya Tongoni, na Shamba la Miti Longuza, hakika kuona ni kuamini, misitu pekeyake ni kivutio tosha cha utalii. Maeneo haya ya mashamba na misitu yanaweza kuimarishwa kwa kuboresha miundombinu ya utalii na kutengeneza mikakati ya masoko kukuza shughuli za utalii,” alisema.
Alisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na TFS, hasa kwenye mikoko iliyopo pembezoni mwa Hoteli ya Tanga Beach, Tongoni na Shamba la Miti Longuza mkoani Tanga, unahitaji kuambatana na hadithi zenye kuvutia zinazoweza kutangaza utalii wa misitu na malikale, huku zikiweka bayana umuhimu wa kulinda mifumo ya ikolojia.
Akieleza zaidi, Mabula alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi wa misitu kwa matokeo bora ya uhifadhi. “Wakati jamii zinapoona manufaa halisi kutoka kwa utalii, kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki katika mazoea endelevu na kulinda mazingira yao,” alieleza.
Kwa kumalizia, Mabula alitoa wito wa ushirikiano kati ya TFS, jamii za ndani, na serikali ili kuendeleza mkakati wa kina wa utalii unaopendelea ukuaji wa kiuchumi na uendelevu wa mazingira. “Kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha kuwa misitu ya Tanzania inabaki kuwa chanzo cha fahari na ustawi kwa vizazi vijavyo,” alihitimisha.
Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, James Nshare, alimshukuru kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS na kueleza kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi.
Aliahidi pia kuimarisha ushirikiano kati ya ofisi zote za TFS na wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi, hususan moto, ambao ni moja ya changamoto kuu katika mashamba na misitu ya hifadhi.