SERIKALI YAOMBWA MALIPO DENI LA BILIONI TANO LA WAFANYAKAZI, WASTAAFU .

Na Mwandishi Wetu,Morogoro

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) , umeiomba Serikali kulipa deni la muda mrefu la malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi , posho na malipo ya wastaafu linalofikia Sh bilioni tano.

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda alitoa hilo ombi katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani Mei Mosi ya mwaka huu (2024) walioyoyaadhimisha Chuoni hapo na kuambatana na kukabidhi zawadi kwa wafanyakazi bora na hodari .

Maadhimisho yam waka huu (2024) ngazi ya mkoa wa Morogoro yamefanyika kwenye halmashauri ya Ifakara Mji, wakati ya kitaifa yakifanyika mkoani Arusha.

Kauli mbiu ya Mwaka huu imasema:”Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha”.

Profesa Chibunda amesema hayo baada ya risala ya wafayakazi iliyosomwa na Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari, Utafiti na Ufundi Stadi,(RAAWU) kwa kushirikiana mwenzake wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) vya matawi katika Chuo Kikuu hicho ambayo ikigusia stahiki za wafanyakazi na ulipwaji madeni ya wafanyakazi.

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu huyo amesema ni kweli wafanyakazi wa Chuo hicho wanaidai Serikali deni la kiasi cha Sh bilioni tano kuanzia mwaka 2017- 2018.

Amesema kati ya fedha hizo, wastaafu wanadai kiasi kinachofikia sh bilioni tatu na wafanyakazi waliopo kazini ( Ofisini) wanadai kiasi cha Sh bilioni mbili.

Profesa Chibunda amesema licha ya madai ya malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu hicho , lakini suala hilo kwa sasa limefanyiwa kazi na tayari asilimia 90 ya madai yameshalipwa.

“ Tayari taarifa za madai haya ameshayafikisha wizara ya fedha na ninawaomba kuwa watulivu wakati madai haya yakiendelea kufanyiwa kazi” amesema Profesa Chibunda.

Katika hatua nyingine amesema wakati Chuo kinashughulikia madai hayo na maslahi mengine , wafanyakazi wa Chuo wanapaswa kujituma kufanya kazi kwa bidii , kujenga tabia ya uadilifu na uwajibikaji sehemu ya kazi.

Profesa Chibunda pia amevitaka vyama viwili vya wafanyakazi ndani ya Chuo hicho kushirikiana ili kuleta maendeleo ya Chuo na Taifa kwa ujumla pasipo kutanguliza maslahi binafsi ya kila chama bali kukitetea chuo na kuitetea nchi yao.

Kwa upande wao, Mwenyikiti wa RAAWU, Faraja Kamendu pamoja na wenzake wa THTU, Dk Nickson Mkiramweni, kwa nyakati tofauti waliushukuru uongozi wa chuo kwa kusaidia madai ya wafanyakazi kulipwa na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi wa kada zote.
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA),Profesa Raphael Chibunda (aliyeshika kamba )akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa viongozi vya vyama vya wafanyakazi  pamoja na kamati ya Maandalizi ya Mei Mosi 2024 ikiwa ni ishara yao ya kutambua mchango wake uliotukukuka katika kuongoza vyema wanajumuiya wa Chuo hicho ambayo ni wafanyakazi na wanafunzi .

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA),Profesa Raphael Chibunda (kati kati walioketi)akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi bora na hodari walichanguliwa kutoka kwenye idara na vitengo katika Chuo Kikuu hicho Mei Mosi ya 2024.

Related Posts