Fadlu amtaja Kibu, Camara | Mwanaspoti

USHINDI wa mabao 3-1 ilioupata Simba juzi dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya katika Kombe la Shirikisho Afrika, umempa mzuka kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ambaye hakuficha hisia zake kwa kuwataja Kibu Denis na Moussa Camara.

Simba imepata ushindi huo na kufuzu hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 3-1, baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Libya kuisha kwa suluhu na kumpa shangwe Fadlu anayeiongoza timu hiyo kwa msimu wa kwanza akirithi mikoba ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Fadlu alisema, amefurahishwa na jinsi wachezaji walivyojitoa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo, huku akisema siri kubwa ya ushindi huo mshambuliaji, Kibu Denis na kipa, Moussa Camara.

“Kila mmoja alitimiza majukumu yake vizuri na hilo ndilo ambalo lilikuwa lengo letu, licha ya wachezaji wengi kukosa uzoefu, nimefurahishwa na ukomavu mkubwa ambao wameuonyesha tangu mwanzoni kutokana na presha iliyokuwepo, hivyo nawapongeza kwa hilo,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Unapopata matokeo ya 0-0 na unarudi nyumbani wapinzani wanapata bao la mapema, kiuhalisia saikolojia ya wachezaji wote inashuka, ila nawashukuru Kibu Denis na Moussa Camara kutokana na kurejesha morali ya wengine na kuendelea kupambana.”

Sababu ya Fadlu kuwapongeza wachezaji hao ni kutokana na Kibu kuifungia Simba bao la kusawazisha baada Cristovao Paciencia Mabululu kuitanguliza Al Ahli Tripoli kabla ya kupiga pia shuti kali la dakika ya 89, lililookolewa kishujaa na kipa, Moussa Camara.

Related Posts