Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeanza kuwaachia wanachama na viongozi wa Chadema waliokamatwa akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Mbali na Mbowe, wengine walioachiwa ni Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, Mwenyekiti Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema na Naibu Katibu Mkuu-Bara, Benson Kigaila.
Mbowe na wenzake wamekamatwa kwa nyakati tofauti asubuhi ya leo Jumatatu, Septemba 23, 2024 wakidaiwa kupanga ama kushiriki maandamano ya Chadema walioyaitisha Septemba 11, 2024.
Maandamano hayo waliyoyaita ya maombolezo na amani yalikuwa na lengo la kupinga matukio ya utekaji, mauaji ya wanachama wa chama hicho na wananchi wengine ambao wamefikwa na kadhia hiyo.
Mapema leo Jumatatu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema wamewashikilia wanachama na viongozi 14.
Usiku wa leo Jumatatu, viongozi na wanachama hao wameanza kuachiwa. Wakili Peter Kibatara amesema Mbowe, Lissu na Lema wameachiwa.
Mtandao wa Kijamii wa Chadema wa X (zamani Twitter) umeandika:” Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe. @freemanmbowetz na Naibu Katibu Mkuu bara Mhe. Benson Kigaila wamepata dhamana katika kituo cha Polisi Oysterbay.
Mwenyekiti bado amebaki kituoni hapo akisubiri wanachama na wananchi wote waliokamatwa wapate dhamana..”
Hata hivyo muda mchache baada ya makada wengine wa chama hicho kuachiwa Mbowe akizungumza na waandishi wa habari alisema watafanya kikao cha viongozi ili kupata maamuzi ya pamoja.
“Kwa sasa usiniulize kama tutaandamana tena au la, mpaka tukae kikao cha pamoja na viongozi ili tuamue kinachofuata,”alisema Mbowe.
Endelea kufuatilia Mwananchi