Walimu kufeli mitihani ya wanafunzi, shida walimu au mfumo?

Katika hali isiyo ya kawaida, walimu wanaweza kufeli mitihani ileile waliyowatahini wanafunzi wao?

Je, hali hii inaweza kuwa kipimo cha kuonyesha kuwa walimu hawa ni wabovu iwapo watastukizwa kufanya mitihani hiyo pasipo maandalizi?

Turejee historia. Tukio hili lilizuka mwaka 2011, wakati aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako, alipowapima ghafla walimu wa darasa la saba kufuatia wimbi kubwa la wanafunzi kufeli mtihani wa Taifa.

Awali, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, aliwasilisha kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana matokeo ya mtihani wa darasa la saba ya mwaka 2011, matokeo ambayo yalionekana kuwa mabovu zaidi kuliko miaka ya nyuma.

Katika hotuba yake, Mulugo alitoa ufafanuzi wa kina juu ya sababu zilizochangia hali hiyo, akisema kuwa kiwango cha ufaulu kilishuka kwa kasi isiyotarajiwa, jambo lililowatia hofu wadau wa elimu kote nchini.

Alikiri kuwa mfumo wa elimu ulikuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi na matokeo hayo yalikuwa ishara dhahiri ya matatizo ya kimuundo na kiutendaji.

Pembeni yake, alikuwapo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Selesine Gesimba, naye akionekana mwenye huzuni kwa matokeo hayo mabaya.

Matokeo ya mtihani huo yalizua mjadala mkali, huku ikifichuka kuwa maandalizi duni ya wanafunzi na ukosefu wa rasilimali muhimu shuleni, vilichangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa viwango vya ufaulu.

Aidha, kulikuwepo na lawama zilizowalenga walimu moja kwa moja kama vile kukosa mafunzo ya kutosha na uwiano duni wa miundombinu ya elimu kati ya shule za mijini na vijijini.

Licha ya changamoto hizo, Serikali ilishinikizwa kuchukua hatua za dharura kurekebisha hali hiyo. Wadau wa elimu waliitaka Serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu, kuhakikisha kwamba walimu wanapata mafunzo ya kisasa na kuweka mazingira bora ya kujifunza kwa wanafunzi, ili matokeo ya baadaye yaweze kurejea katika viwango vya kuridhisha.

Walimu wafanyishwa mtihani

Walimu ambao walitarajiwa kuwa na ujuzi wa kutosha kuwanoa wanafunzi, walijikuta wakiwa chini ya kipimo hicho muhimu alichokitumia Dk Ndalichako.

Matokeo yao, hata hivyo, yalikuwa ya kushangaza kwani wengi wao walifeli kwa kiwango cha kushangaza, jambo lililoibua mijadala mkali miongoni mwa wadau wa elimu.

Kushindwa kwa walimu hao kulitikisa tasnia ya elimu, huku kukiwa na maswali mengi juu ya ubora wa walimu shuleni.

Wadau wa elimu na wazazi walichukulia tukio hilo kama ishara ya udhaifu katika mfumo mzima wa mafunzo ya walimu.

“Kama walimu hawawezi kufaulu mitihani wanayoitegemea kuandaa wanafunzi, kuna tatizo kubwa,” alisema mmoja wa wazazi waliokuwa wakifuatilia kwa karibu matokeo hayo.

Hali hii ililazimisha Serikali na vyombo husika kuangalia upya mbinu za mafunzo ya walimu na kufanya marekebisho ya kina katika sekta ya elimu, ili kuhakikisha walimu wanakuwa na uelewa wa kutosha wa mitalaa wanayofundisha.

Kikwete akumbushia machungu

Hivi karibuni ilisambaa video katika mitandao ya kijamii ikimuoonesha Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akihojiwa katika televisheni moja, akirejea tukio hilo la walimu kufanyishwa mtihani.

Alieleza namna ambavyo hata walimu mara nyingine hutunga mitihani ambayo hawana uwezo nayo.

Rais Kikwete alifafanua ugumu uliopo katika utoaji wa elimu nchini, huku akiwashutumu baadhi ya walimu kwa kukosa weledi katika utendaji wao wa kazi.

Alisema wakati akiwa madarakani aliitisha kikao na Ndalichako, aliyemueleza kuwa ufaulu mbaya ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na walimu, huku akithibitisha kauli hiyo kwa utafiti mdogo alioufanya kwa baadhi ya walimu kwa kuwapatia mitihani hiyo hiyo na kisha kufeli.

“Pamoja na kuwa walikwishaiona mitihani hiyo, ajabu walifeli vibaya sana, hii inaonesha kuna shida mahali kwani hata wao wanaweza kuwa wanafundisha mada wasizozifahamu vema,”alisema Rais huyo huku akiangua kicheko.

Kauli ya Rais Kikwete ilipokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya walimu, huku wengi wao wakisema suala la ufaulu wa wanafunzi halichangiwi na walimu pekee.

Walisema kufeli ni mkusanyiko wa mambo mengi ikiwemo miundombinu, motisha na uwezo wa akili wa wanafunzi husika.

Mwalimu Ngwanaeliza Paul wa shule moja ya msingi jijini Arusha anasema kufanya mtihani sio tatizo, huku akifafanua kuwa upimaji wowote unahitaji maandalizi hata kama anayetakiwa kuufanya ni mwalimu.

‘’Mwalimu anafundisha, kuwaandaa na kuwelekeza wengine. Inatofautiana na kufanya mtihani tena kwa mada zote,’’ anasema.

Mwalimu Bariki Urassa wa mkoani Kilimanjaro anasema: “Mtihani ni mtihani tu’ mtahiniwa yeyote awe mdogo au mtu mzima, lazima ajiandae. Tumesoma na wazee chuo kikuu tena wazoefu wa muda mrefu, lakini walikuwa wakihangaika na pengine hadi kutazamia mitihani, ilhali maswali yaliyokuwa yakiulizwa ni yaleyale waliyokuwa wakiyafanyia kazi kila siku kazini.’’

Mwalimu huyo anaongeza kusema kuwa mara zote walimu wa shule za umma wana nafasi kubwa ya kufeli mitihani ya darasa la saba, kwa sababu mara zote hufundisha kimazoea tofauti na walimu wa shule za binafsi ambao ikitokea mwalimu anafanya madudu huondeolewa kazini.

Mwaka 2016, tukio lililozua gumzo nchini Nigeria lilijitokeza katika jimbo la Kaduna, baada ya maelfu ya walimu wa shule za msingi kushindwa kufikisha viwango vya ufaulu walipofanyiwa mtihani ulioandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wenye umri wa miaka sita na saba. Gavana wa jimbo hilo, Nasir El-Rufai, alithibitisha kuwa walimu 21,780 kati ya waliowekwa kwenye jaribio hilo walishindwa kufikia asilimia 75 ya alama za ufaulu.

Katika hotuba yake kwa wawakilishi wa Benki ya Dunia, El-Rufai alisema kuwa walimu hao waliondolewa mara moja kutoka kwenye ajira zao, hatua iliyosababisha serikali ya jimbo kuanza mchakato wa kuajiri walimu wapya wapatao 25,000 kwa ajili ya kuziba pengo hilo.

“Mpango wa ajira wa awali ulikuwa wa kisiasa,” alisema El-Rufai, akinukuliwa na gazeti la Daily Trust la Nigeria, akiongeza kuwa: “Serikali imejipanga kubadili mfumo huo kwa kuajiri walimu wenye sifa stahiki ili kurudisha hadhi ya elimu katika jimbo letu.”

Tukio hili lilizua maswali mengi kuhusu viwango vya elimu nchini Nigeria, huku wadau wa sekta ya elimu wakilalamikia jinsi mfumo wa ajira kwa walimu, ulivyokuwa ukiendeshwa kwa misingi ya kisiasa badala ya ufanisi wa kitaaluma.

 Wakati serikali ilipochukua hatua hii kali, ilizua mijadala miongoni mwa wananchi, huku baadhi wakiiunga mkono ikisema ni hatua sahihi kwa manufaa ya elimu ya watoto wa Kaduna, wakati wengine wakieleza wasiwasi kuhusu uwezo wa serikali kujaza nafasi hizo za walimu kwa wakati.

Mwalimu anawezaje kufeli?

Walimu wanaweza kufeli mitihani ya masomo wanayofundisha? Nini kinaweza kusababisha walimu kushindwa mitihani hiyo, licha ya kuwa wanafundisha wanafunzi wao kila siku?

Mambo kadhaa yanaweza kuchangia hali hii, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa maandalizi thabiti kwa walimu hao kabla ya kufanyiwa mtihani ghafla.

Mwalimu anayetarajiwa kufundisha darasa la saba, kwa mfano, anaweza kukosa muda wa kujiandaa vizuri kutokana na ratiba ngumu ya kazi au mbinu anazotumia kufundishia ambazo zinaweza kuwa si sahihi kulingana na mahitaji ya mitihani ya kitaifa.

Nchini Singapore, walimu hupimwa uwezo wao mara kwa mara ili kuhakikisha wanabaki kuwa na viwango vya juu vya kitaaluma.

Dr. Pasi Sahlberg, mtaalamu wa elimu kutoka Australia, anaeleza kuwa walimu bora lazima wawe na ujuzi wa kina wa mitaalaa wanayofundisha ili kuwasaidia wanafunzi wao kufaulu.

 Sahlberg anaongeza kwamba walimu ambao hawana ujuzi wa kutosha huishia kuwafanya wanafunzi kushindwa mitihani, hali inayodhuru mfumo mzima wa elimu.

Nchini Kenya, mfumo wa kuwapima walimu kupitia mtihani unaojulikana kama Teacher Proficiency Test (TPT) umeonesha kuwa walimu wenye uwezo wanaweza kutoa elimu bora, lakini pia umeonesha kwamba walimu wasiokuwa na maandalizi ya kutosha wanashindwa kufaulu mitihani hiyo.

Profesa John Hattie wa Chuo Kikuu cha Melbourne, Australia, anaamini kuwa mfumo wa kuwapima walimu mara kwa mara unasaidia kuinua viwango vya elimu, akisema, “Hakuna mafanikio katika elimu bila walimu wenye uwezo.”

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba kushindwa kwa mwalimu kufaulu mtihani wa masomo wanayofundisha, siyo kiashiria pekee cha kutokuwa na uwezo au kufaa kwa kazi. Maandalizi ya mtihani, hali ya kitaaluma na mazingira ya kazi, vinapaswa kuchukuliwa kama sehemu ya tathmini, badala ya kuhukumu moja kwa moja uwezo wa mwalimu kwa kalamu na karatasi.

Related Posts