Matumaini lukuki wananchi wa Madaba utekelezaji wa mradi wa maji

Madaba. Huenda changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji ikabaki historia katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma, baada ya Serikali kutekeleza Mradi wa Maji wa Mtyangimbole katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, kabla ya kukamilika kwa mradi huo, wanategemea maji ya visima vya watu binafsi.

Mradi huo unaotarajiwa kuvinufaisha vijiji vinne ni miongoni mwa miradi 30 inayotekelezwa wilayani humo.

Leo, Jumanne Septemba 24, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo.

Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Kijiji cha Mtyangimbole, Zainabu Kanyale amesema kwa sasa hawana uhakika na usalama wa maji wanayotumia.

“Tunachota maji kwenye visima vya watu binafsi, lakini huwa vinakauka kwa hiyo, tutakwenda kuchota mabondeni. Hayo ya mabondeni ni machafu na wanatumia wanyama wengine pia,” amesema.

Ingawa wanategemea maji kutoka kwenye visima vya watu binafsi, Zainab amesema pia, havina uhakika kwa kuwa nyakati za jua vinakauka.

Hata hivyo, amesema katika visima hivyo wanatozwa Sh5,000 kwa mwezi na wengine zaidi ya hiyo.

“Lakini kuna wakati hupewi maji na ili kuepuka kusumbuliwa ndiyo tunaenda mabondeni,” ameeleza.

Zainab amesema mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo katika kijiji hicho, hivyo watakuwa na uhakika wa maji.

“Tumeona mradi unatekelezwa, tunaanini ukikamilika nasi tutakuwa na maji nyumbani,” amesema.

Aprili Milano, mkazi wa eneo hilo, naye amesema ni matumaini yake, kukamilika kwa mradi huo utakaowaondoa kwenye changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.

“Ni muda mrefu tulikuwa tunaangaika na maji, ukiamka jambo la kwanza unawaza nitapata wapi maji, lakini kuna dalili njema sasa,” amesema.

Mbali na Kijiji cha Mtyangimbole, mradi huo unaotekelezwa kwa Sh5.5 bilioni utavinufaisha vijiji vingine vya Luhimba, Likalangilo na Gumbilo.

Ratiba ziara ya Rais Samia leo

Sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi huo, Rais Samia anatarajiwa pia kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la nafaka la Luhimba.

Uwekaji wa jiwe la msingi katika ghala hilo unawakilisha maghala mengine 28 yanayojengwa mkoani Ruvuma.

Baada ya hatua hiyo, mkuu huyo wa nchi atazindua Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Chifu Zulu.

Kisha ratiba ya ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma kwa leo, itahitimishwa na mazungumzo na wafanyakazi wa shamba la kahawa la Aviv Tanzania Limited mkoani Ruvuma.

Related Posts