Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za saratani na vifaa tiba ili kutanua wigo wa huduma za saratani nchini na hivyo kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Pia ametoa rai kwa uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha wananchi wote bila kujali dini, kipato na itikadi zao wanapata huduma hizo muhimu za afya.
Dk. Biteko amesema hayo leo tarehe 2 Mei 2024 wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa Kituo cha Matibabu ya Saratani cha Aga Khan, Jijini Dar es Salaam.
“Serikali yetu imejipanga kuboresha huduma za afya na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na mfano wa juhudi hizi ni Serikali kutenga eneo kilipojengwa kituo hiki ambacho kimepanga kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku kwa matibabu ya mionzi, wagonjwa 25 kwa siku kwa tiba za kemikali na wagonjwa 25 kwa siku kwa uchunguzi wa saratani na huduma za chanjo,” amesema Dk. Biteko.
Dk. Biteko ametoa rai kwa uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha wananchi wote bila kujali dini, kipato na itikadi zao wanapata huduma hizo muhimu za afya.
Aidha, ameupongeza Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) kupitia Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan Tanzania kwa ushirikiano na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) pamoja na Kituo cha Tiba Bugando (BMC) kwa kubuni mradi shirikishi kati ya sekta ya umma na sekta binafsi uitwao Mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na saratani.
Ameeleza kuwa, mradi huo wenye thamani ya jumla ya Euro milioni 13.3 (Sh 35 bilioni) umekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya miaka minne ya utekelezaji wake ikiwemo kutoa mafunzo kwa wahudumu 464 na watumishi 400 ngazi ya jamii kuhusu huduma za saratani.
Kupitia mradi huo wanajamii zaidi ya milioni 4.5 wamepewa elimu kuhusu saratani, watu takriban 700,000 wamepimwa saratani na zaidi ya wagonjwa wapya 39,093 kugunduliwa kuwa na saratani kupitia vipimo stahiki na hivyo kuwawezesha kuanza kupata tiba stahiki.
Pia ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali za afya nchini kuhakikisha zinajikita pia kwenye kuzuia ugonjwa wa saratani kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya afya na lishe kwani wataalam wanaamini kuwa magonjwa hayo yanaweza kuepukika na hivyo kuepusha gharama kubwa zinazotumika kwenye matibabu.
Pia ametoa agizo kwa kituo hicho cha Aga Khan kushirikiana na vituo vingine vya matibabu ya Saratani nchini hususan Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji madhubuti wa huduma za tiba za mionzi na hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa Ocean Road.
Dk. Biteko ameuhakikisha uongozi wa Hospitali ya Aga Khan kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wao katika utoaji wa huduma za afya hasa kwenye magojwa yasiyoambukiza na kwamba ipo tayari kutoa ushirikiano kwao muda wote.
Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kuwa changamoto ya saratani nchini ni kubwa ambapo kila mwaka kuna wagojwa wapya 40,000 huku vifo 27,000 na kwamba saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 23.5.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya saratani ikiwemo kuboresha miundombinu, kununua vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalam wa matibabu ya saratani ambapo mwaka huu ametoa Sh 10 bilioni kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa na madaktari wabobezi kwenye masuala ya saratani.
Amesema uboreshaji wa huduma za afya nchini unaendelea ili kutimiza dhima ya Rais Samia ya kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha utoaji wa huduma za kisasa za afya kwa wananchi ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan, Mwana Mfalme, Zahra Aga Khan amesema kujengwa kwa kituo hicho ni ushahidi wa namna Tanzania inavyopiga hatua kwenye Sekta ya Afya kwa kutumia pia teknolojia ya hali ya juu ya kisasa kwenye matibabu.