Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeipa Serikali ya Tanzania siku 14 kuwasilisha majibu na kiapo kinzani katika shauri la kupinga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Novemba 27, 2024 na Agosti 15, mwaka huu mchakato wa uchaguzi huo utaanza.
Lakini wanaharakati watatu wanaojitambulisha ni raia wa Tanzania waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, wamefungua shauri la kuupinga kwa utaratibu wa mapitio ya Mahakama.
Shauri hilo limefunguliwa na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe, mwanahabari mstaafu, Ananilea Nkya na Bubelwa Kaiza na wajibu maombi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika shauri hilo linalosikilizwa na Jaji David Ngunyale, wanaharakati hao wanapinga kanuni za uchaguzi huo za mwaka 2024 zilizotungwa na Waziri wa Tamisemi, wakihoji mamlaka yake.
Pia, wanapinga uchaguzi huo kusimamiwa, kuratibiwa na kuendeshwa na Ofisi ya Rais Tamisemi, badala ya Tume Huru ya Uchaguzi, kwa mujibu wa Sheria ya Tume huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.
Shauri hilo, limetajwa leo Jumanne, Septemba 24, 2024 kwa mara ya kwanza. Wajibu maombi kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a wameomba wapewe muda wa siku 14 kwa mujibu wa sheria wa kuwasilisha majibu yao pamoja na kiapo kinzani.
Wakili wa waombaji hao, Jebra Kambole amepinga hilo la siku 14 akidai ni muda mrefu huku akiiomba Mahakama hiyo ipange kusikiliza shauri hilo haraka, hoja ambayo pia imepingiwa na Wakili Chang’a akitaka matakwa ya sheria yazingatiwe.
“Mheshimiwa jaji, waombaji baada ya kupata kibali walipewa siku 14 na wamezitumia zote, kwa hiyo na sisi tunaomba siku 14 kama sheria inavyoelekeza ili tuweze kuwasilisha majibu ya maombi sambamba na kiapo kinzani,” amesema Wakili Chang’a.
Jaji Ngunyale baada ya kusikiliza hoja za pande zote amekubaliana na ombi la wajibu maombi na kutoa siku 14 kuwasilisha majibu yao pamoja na kiapo kinzani.
Hivyo, Jaji Ngunyale ameelekeza wajibu maombi kuwasilisha majibu yao pamoja na kiapo kinzani kabla au Oktoba 7, 2024.
Pia, amepanga shauri hilo kutajwa Oktoba 7 asubuhi kwa ajili ya kuangalia kama inaweza kuanza usikilizwaji siku hiyo mchana au la.
Wanaharakati hao walifungua shauri hilo baada ya kuomba na kupata kibali cha Mahakama kilichotolewa Septemba 9, 2024 na Jaji Wilfred Dyansobera aliyesikiliza shauri hilo la maombi ya kibali hicho.