MKWAWA WAADHIMISHA WIKI YA TISA YA UTAFITI NA UBUNIFU – MWANAHARAKATI MZALENDO

NA EMMANUEL MBATILO

VYUO Vikuu vina jukumu kubwa la kuwa injini ya ubunifu na ugunduzi kwani ni kitovu cha uzalishaji wa maarifa, ambapo tafiti bora za masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisayansi hufanywa na mawazo ya mabadiliko huzaliwa.

Hata hivyo, ili mawazo haya yaweze kuzaa matunda, lazima yatafsiriwe vizuri kwenye mahitaji halisi ya taifa na dunia kwa ujumla kupitia ushirikiano na washirika wa sekta mbalimbali na viwanda.

Ameyasema hayo Aprili 18, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, Prof. Joseph Ndunguru wakati akifungua Maadhimisho ya Tisa ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ngazi ya Chuo Kishiriki Cha Elimu Mkwawa mkoani Iringa.

Amesema sekta mbalimbali na viwanda, kwa upande mwingine, huleta rasilimali muhimu, utaalamu, na changamoto halisi ambazo makundi yote mawili (yaani wanataaluma na wataalam kwenye viwanda) wana wajibu wa kuzijadili na kutafuta suluhisho.

“Kwa kushirikiana na vyuo vikuu, viwanda hupata maarifa yenye mitazamo mpya kwenye uendeshaji wa viwanda. Hivyo basi, ushirikiano wa wanataaluma na wataalam kwenye viwanda husaidia kuziba pengo kati ya nadharia na mazoezi, kugeuza dhana za kufikirika kuwa suluhisho halisi la changamoto kwenye taifa na ulimwengu kwa ujumla”. Amesema Prof. Ndunguru.

Aidha Prof. Ndunguru ameipongeza Menejimenti ya Chuo kwa kuendelea kutenga fedha kila mwaka ili kugharamia shughuli za utafiti na ubunifu kwa wafanyakazi wake.

Vilevile amewapongeza kukamilisha ujenzi wa Maabara ya Biolojia na mipango mbalimbali mliojiwekea kwenye ujenzi wa miundombinu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

“Ujenzi wa maabara na majengo mengine kupitia mradi huu vitasaidia kuendelea kuboresha tasnia ya utafiti hapa chuoni na kukiwezesha Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa kuendelea kusaidia katika utatuaji wa changamoto mbalimbali ambazo zinalikabili Taifa letu ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kufikia uchumi wa viwanda”. Amesema

Pamoja na hayo amesema kuwekeza kwenye miundombinu ya utafiti, kukuza ujuzi wa mbinu za ujasiriamali, pamoja na kusisitiza ujuzi wa teknolojia ya kisasa miongoni mwa wanafunzi wetu.

“Mambo haya yatasaidia kukuza utamaduni kwa wanafunzi wetu kudadisi vitu na hatimaye kuchochea ubunifu na uvumbuzi kupitia tafiti mbalimbali”. Ameeleza Prof. Ndunguru.

Kwa upande wake Kaimu Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Prof. Deusdedit Rwehumbiza amesema ujenzi wa maabara ya biolojia umekamilika na Chuo kimeshakabidhiwa maabara hiyo na imeanza kutumika.

Amesema Maabara hiyo imekisaidia Chuo kuongeza nafasi kwa wanafunzi na wafanyakazi kufanya majaribio mengi ya kisayansi.

“Maabara hii inawasaidia wanataaluma wetu pamoja na wanafunzi kufanya tafiti na kujifunza kwenye mazingira rafiki. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutusaidia kukamilisha upanuzi wa maabara hii”. Amesema Prof. Rwehumbiza.

Pia amesema kuwa Chuo kimefanikiwa kukamilisha ujenzi wa jengo la ofisi ya masuala anuwai (Gender Diversity) ambalo litakisaidia Chuo kuongeza ufanisi katika kukabiliana na changamoto zinazohusisha unyanyasaji wa kijinsia wakati wa utekelezaji wa shughuli za msingi za Chuo, zikiwemo shughuli za utafiti na ubunifu.

Hata hivyo amesema kuwa Chuo kimesaini mkataba wa ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kila moja, na ujenzi wa maktaba ya Chuo yenye uwezo wa kuchukua watumiaji 1,500 tofauti na maktaba iliyopo ambayo ina uwezo wa kuchukua watumiaji 500.

“Kukamilika kwa mabweni ya wanafunzi kutakisaidia Chuo kutoa huduma ya malazi kwa wanafunzi 1,750 (30.1%) kutoka wanafunzi 1,150 (19.8%) wanaopata huduma hiyo kwa sasa”. Amesema

Sanjari na hayo amesema kuwa ujenzi wa maktaba mpya utakisaidia Chuo kuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya watumiaji 2000 ambao ni 33.3% ya idadi ya wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo wapatao 6,000 ikilinganishwa na maktaba iliyopo ambayo uwezo wake ni 8.3%.



Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *