Morogoro. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Said Aboud amebainisha umuhimu wa matokeo ya tafiti zinazofanyika kuwasilishwa kwa watunga sera na wafanya uamuzi ili kuboresha huduma za afya.
Pia, amesisitiza tafiti hizo zitafsiriwe katika lugha nyepesi inayoeleweka kwa wananchi ili waelewe namna zinavyoweza kuwasaidia.
Profesa Aboud amebainisha hayo leo Septemba 24, 2024 mjini Morogoro baada ya kufungua mkutano wa kujadili vijarida sera vilivyoandaliwa na NIMR na kuwasilishwa kwa watafiti, watunga sera, wafanya uamuzi na wataalamu kutoka programu za Wizara ya Afya za Ukimwi, magonjwa ngono, malaria na kifua kikuu.
Amesema uzoefu unaonesha kuna tafiti nyingi za kisayansi zinafanyika hapa nchini na zina matokeo mazuri, lakini matokeo hayo yanabaki kwenye machapisho, hayatumiki kusaidia kutunga sera na kufanya uamuzi katika kuboresha huduma za afya.
“Kama taasisi tunafanya tafiti zinazotoa matokeo au ushindi wa kisayansi, sasa ili matokeo hayo yaweze kutumika ipasavyo, inabidi yatafsiriwe kwa lugha nyepesi ambayo hata mwananchi wa kawaida anaweza kufahamu,” amesema Profesa Aboud.
Mtafiti mkuu na mkuu wa kitengo cha tafiti za mifumo ya afya, sera na uchakataji wa matokeo ya kitafiti, Dk Elizabeth Shayo amesema majadiliano ya ushahidi wa tafiti mbalimbali za kisayansi yanasaidia kuboresha sera na uandaaji wa miongozo ya utoaji wa huduma za afya nchini.
Dk Shayo amesema kupitia majadiliano itasaidia kufanya uchanganuzi na kuangalia tafiti zilizofanyika katika nchi mbalimbali zinazoweza kutumika katika kuboresha huduma za afya.
Amesema NIMR imepewa dhamana ya kufanya utafiti wa magonjwa ya binadamu kwa niaba ya Wizara ya Afya na Serikali, kwa lengo la kutoa matokeo ya ushahidi kisayansi wa magonjwa hayo.