Dar es Salaam. Mwili wa mwanamume ambaye bado hajafahamika jina lake, umekutwa ndani ya gari ya Range Rover, eneo la Magomeni Mapipa wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Gari hilo lilikokuwa limeegeshwa Magomeni, halina namba ya usajili wa Tanzania.
Eneo lililokuwa gari hilo ni maarufu kwa uuzaji wa magari ya aina mbalimbali ambayo huegeshwa kwa ajili ya kutafuta wateja.
Mwananchi limefika katika eneo hilo kuanzia jioni ya 11 leo Jumanne, Septemba 24, 2024 na kukuta wananchi wamejazana wakisubiri polisi kufika.
Baada ya kufika askari polisi wamefanya jitihada za kufungua milango ya gari kitendo kilichochukua zaidi ya nusu saa hadi kufanikiwa kuifungua.
Kabla ya baada ya kuifungua milango ya gari hilo askari polisi na watalaamu wa afya waliokuwa hapo walilazimika kupuliza dawa ili kupunguza harufu iliyokuwa ikitoka katika gari hilo.
Baada ya kufanikiwa kufungua mlango, mwili wa mwanamume huyo ulikuwa eneo la buti ukiwa kifua wazi huku simu yake janja ikiwa katika miguu yake.
Kwa namna polisi walivyoufungua mlango wa buti mwili wa mwanamume ulionekana kama umelala kwa staili ya kujikunja huku ukiwa umevimba.
Baadhi ya mashuhuda waliozungumza na Mwananchi wamesema gari hilo lina siku ya tatu tangu kuegeshwa katika eneo hilo na walivyoliona hawakutilia shaka kwa sababu ni eneo linalouzwa magari.
“Asubuhi kulikuwa shwari hakukuwa na harufu yoyote, lakini kuanzia mchana hadi jioni nilivyokuwa nabeti (kubashiri), nikasikia harufu kali tukajiuliza kuna nini au paka mmoja kafa maana kuna paka wengi hapa.
“Hakutujua kama ndani ya gari kuna mtu, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda tukaanza kutafuta huyo paka, kilichotushtua ni inzi wengi kuwepo katika gari ndipo tukagundua kuwa kuna mwili,” anasema Hamis Hamad anayeishi Magomeni.
Masoud Ally amesema:”Gari hili lipo tangu siku ya mechi ya Yanga na CBE (Jumamosi Septemba 21, 2024), wakati napita asubuhi sikuisikia harufu lakini kuanzia jioni hali ilibadilika jambo lililozua hofu kwa wapita njia.”
Polisi pamoja watalaamu wa afya wameshauchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.