DC Chunya aagiza waliovamia eneo la mradi wa BBT kuondoka

Chunya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mubarak Batenga ameagiza kaya 52 za jamii ya wafugaji zilizovamia eneo la mradi wa kilimo cha soya Kijiji cha Masiano wilayani humo, kuondoka mara moja.

Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 52,000, limetengwa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kujenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kwa vijana kuwekeza uzalishaji wa  soya.

Batenga ameiambia Mwananchi leo Septemba 24, 2024 ikiwa ni siku chache baada ya kufanya mkutano wa hadhara kwa wananchi wa kijiji hicho na kutoa maelekezo ya Serikali.

“Waliovamia eneo la mradi wa kilimo cha soya lazima waondoke kupisha utekelezaji wake ambao utaanza wakati wowote kuanzia sasa kupitia udhamini wa Benki ya Dunia,” amesema.

Batenga amefafanua kuwa, mradi huo wa BBT ni mkubwa na unakwenda kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana huku akisisitiza kujipanga kunufaika na uwekezaji huo wa Serikali.

“Kilimo cha soya kitawanufaisha wananchi hususan vijana wa vijiji vya Masiano na Mapogoro wilayani humo ni vyema kuanza kujiweka sawa kupokea mradi huo ili kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Batenga amesema kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, Serikali imetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 2,594 katika vijiji vya Mapogolo na Shoga kwa ajili ya jamii ya wafugaji sambamba na waishio Kijiji cha Masiano.

“Eneo hilo ni mahsusi kwa wafugaji wa vijiji vya Masiano na Mapogoro ambao wataondolewa kupisha mradi wa kilimo cha soya kupitia uwekezaji wa Kujenga Kesho Iliyo Bora (BBT),” amesema.

Amewaonya wananchi kuepuka kuvamia maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi badala yake wayalinde na kuyaheshimu.

Batenga amesema umefika wakati Watanzania waheshimu mpango wa Serikali wa matumizi bora ya ardhi ili kujiletea maendeleo na wasiwe chanzo cha migogoro isiyokwisha.

Mkazi wa Kijiji cha Masiano, Shija Furaha ameomba Serikali kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara, elimu, kukosekana kwa zahanati ya kijiji, nishati ya umeme na maji.

“Tunaomba Serikali sikivu isaidie jamii kupata huduma muhimu kwani wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya na elimu kwa vijana,” amesema.

Kwa upande mwingine, amesema wamepokea agizo la Serikali la kuondoka katika eneo linalotekelezwa mradi wa BBT huku wakiomba watakaoguswa kupewa kipaumbele.

Awali, Batenga aliwaondoa hofu wananchi kwa kueleza maeneo ambayo Serikali imetenga kwa ajili ya jamii ya wafugaji, huduma muhimu zitaboreshwa ikiwamo kujenga miundombinu ya elimu, maji, barabara na nishati ya umeme.

Related Posts