Unayakumbuka mabasi ya ‘kumbakumba’ | Mwananchi

Wahenga wa Dar es Salaam, hawatosahau usafiri wa mabasi ya ghorofa na yale ya Ikarus maarufu kwa jina la ‘kumbakumba’.

Ikarus yalikuwa mabasi marefu yakimilikiwa na lililokuwa Shirika la  Usafiri Dar es Salaam au maarufu kwa kifupi cha Uda.

Yaliitwa kumbakumba kwa namna yalivyokuwa yakichukua idadi kubwa ya abiria kama ilivyo sasa kwa baadhi ya mabasi ya mradi wa mwendo kasi.

Moja ya raha zilizokuwamo katika mabasi haya kiasi cha kuwavutia abiria wengi ni ule muundo wake wa kutengenezwa ambao uliruhusu gari likiwa barabarani kunesanesa, hivyo kuwapa raha abiria.

Kwesa Kwesa anaeleza kuwa japo hakuyafaidi sana mabasi hayo kwa kuwa alikuwa mdogo miaka hiyo, lakini mwonekano wake ulikuwa unawavutia wengi.

“Ukitazama ule urefu wake na yanavyonesanesa hasa pale kwenye maungio, ilikuwa raha sana. Kizazi cha sasa angalau na wao wanayaona kwa kupitia haya mabasi ya mwendokasi, lakini kwa zamani mabasi yale yalikuwa ni zaidi ya kupanda kwa kweli,’’ anasema.

Anahoji kama kuna kumbukumbu yoyote ya aina hiyo ya mabasi hapa nchini… “Najua mwendo kasi yapo mabasi ya muundo huo, lakini hizi ikarusi zetu basi wangeziweka makumbusho. Uongozi wa jiji ulichukulia kwa umakini hili jambo,’’ anasema.

Kwa upande wa mabasi ya ghorofa, haya yalikuwa machache sana na  yanaelezwa kuwa yalifanya kazi zaidi  kabla ya uhuru  na baadaye hadi mwaka 1967.

Kituo cha mabasi hayo kilikuwa eneo la Stesheni na yalipita barabara ya Uhuru enzi hizo ikijulikana kwa jina la Kichwele na yaliishia Ilala eneo ilipo shule ya watu wasiosikia. Inaelezwa pia yalikuwa yakipita barabara ya Morogoro kuelekea Magomeni.

Kwa miaka hiyo usingeweza kuona mabasi ya aina ya ikarus au ya ghorofaa hiyo yakienda nje ya njia hizi, kwa sababu hivi ndivyo vilikuwa viunga vya mji wa Dar es Salaam.

Maeneo mengi ya pembezoni zaidi miaka hiyo yalikuwa ni mapori yenye barabara za vumbi.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts