Viongozi SMZ watekeleze kwa vitendo ahadi zao

Utawala wa demokrasia, haki na usawa hupimwa siyo kwa kuwa na Katiba nzuri au kauli za kuvutia, bali kwa vitendo vinavyoonekana uwanjani.

Kwa maana nyingine kigezo ni vitendo na siyo maandishi yaliyomo kwenye Katiba na sheria za nchi. Hii ndiyo sababu iliyowafanya wahenga kutuambia “Ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo.”

Katika kusisitiza maana ya kauli hii, watunzi wa mashairi na nyimbo wametumia msemo huu kusisitiza mantiki ya kauli nzuri kutafsiriwa kwa vitendo na siyo maneno yanayotoka mdomoni kuwa tofauti na yaliyofichwa moyoni.

Miongoni mwa waliosisitiza uzito wa usemi huu ni mwimbaji taarab maarufu wa Zanzibar, Zuhura Shaabani katika wimbo wake usemao Mja Kunena, Muungwana ni Vitendo, ambao ndani yake analalama anachokiona ni kinyume na ahadi aliyopewa.

Katika hizo zinazoitwa juhudi zinazofanyika Zanzibar za kuimarisha demokrasia, mara nyingi huukumbuka usemi huu wa wahenga na wimbo wa Zuhura.

Hii ni kwa sababu yanayofanyika dhahir shahir, mchana kweupe, ni kinyume na ahadi iliyowekwa katika Katiba na sheria, zikiwemo zile zinazoongoza siasa za mfumo wa vyama vingi.

Kinachofanyika ni kama vyama vimegawanywa katika makundi tafauti, moja la dhahabu na mengine ni ya fedha na shaba na ndiyo maana wengine wanabanwa kulia na kushoto kufanya shughuli zao za kila siku.

Kwa mfano viongozi wa CCM hawawekewi vikwazo kutembelea miradi ya Serikali, shule au taasisi za umma na kuzungumza na wafanyakazi au wanafunzi. Lakini inakuwa mwao wenzao wa ACT Wazalendo wanapotaka kufanya hivyo. Tukumbuke miradi na taasisi za umma zinaendeshwa kwa kodi za raia na siyo wanaCCM peke yao.

Hata viwanja vya shule vinatumiwa bila ya matatizo na CCM, lakini ACT Wazalendo wanawekewa vikwazo na wakipenya katika tundu ya sindano, wanaowaruhusu hukiona cha mtema kuni.

Hivi karibuni, walimu wakuu kisiwani Pemba walionywa na kupewa uhamisho bila ya maelezo, lakini wakaambiwa walijipalia makaa kwa kuwapa ACT Wazalendo kumbi za shule kufanya mafunzo.

Hata vyombo vya habari vinavyoitwa vya umma havitoi nafasi sawa na ni mara chache utasikia habari za vyama vya upinzani, hata vinapofanya uchaguzi. Lakini kiongozi wa CCM akitoa msaada wa kujenga choo cha shule, huwa habari kubwa.

Hali hii haiimarishi demokrasia na utawala bora na hayo yaliyotajwa kama maridhiano yaliyosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), yanaonekana ni ya makaratasi tu.

Najua wapo watakaonuna kwa kuyaeleza haya, lakini kama hawayapendi wasingeyafanya. Mfano mwingine ni watu wote wanaochagua wawakilishi wa serikali katika mitaa na vijiji (masheha) ni wakereketwa wa CCM.

Tujiulize, hivi hakuna mwanachama wa ACT Wazalendo au chama kingine cha siasa isipokuwa CCM chenye uwezo wa kuifanya kazi hii?

Sasa bado mwaka mmoja kufanyika uchaguzi wa saba wa mfumo wa vyama vingi na zipo dalili kwamba utakuwepo msuguano kama katika chaguzi zilizopita, hasa kwa kuwa wengi watakaousimamia ni wale waliolalamikiwa kuvuruga chaguzi zilizopita.

Masuala haya na kura ya mapema inayodaiwa na wapinzani kuwa mkakati wa kupata uwanja wa kufanya mizengwe, kama hayajapatiwa ufumbuzi yanaweza kuirejesha Zanzibar kwenye matatizo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliahidi kwamba atahakikisha uchaguzi ujao utakuwa safi, huru na wazi, lakini yanaonekana ni maneno na siyo vitendo.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inapofanya mikutano ya waandishi wa habari kuelezea kazi zake, utaona waandishi maalumu ambao hawaulizi maswali magumu au yanayohitaji ufafanuzi, hao ndio wanaoalikwa.

Wale wasiokuwa na muhali katika kuutafuta ukweli na kuonyesha dosari zilizopo wanatengwa kwa vile wataweka wazi kile kinachodaiwa kuwa uovu katika matayarisho ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Zanzibar ni yetu sote na kila mwenye kuipenda anataka amani ya kweli na utulivu na njia mojawapo ni kuona Katiba inaheshimiwa kwa vitendo na kunakuwa na uwanja sawa kwa vyama vya siasa na uhuru wa kujieleza.

Katika wakati huu, ni muhimu kwa Serikali kutimiza ahadi ya Rais Mwinyi ya kufanya marekebisho ya sheria ya habari na uhuru wa kujieleza aliyoitoa mara tu alipoingia madarakani.

Wadau wa habari wamechoka kusubiri utekelezaji wa hiyo ahadi. Kinachofanyika ni kila siku kupigwa danadana kama afanyavyo kuku kwa kifaranga chake kinapotaka kunyonya.

Wiki iliyopita kikao cha Baraza la Wawakilishi kilianza vikao vyake ambapo marekebisho ya kapu la sheria yaliwasilishwa, lakini marekebisho ya sheria ya habari hayamo na haijaelezwa lini yatafanyika.

Sijui hofu ipo wapo na sasa ni miaka 20 tangu madai hayo ya marekebisho yalipoanza na Serikali kuahidi kwamba itairekebisha. Tukumbuke usemi wa busara za wahenga “Ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo”.

Related Posts