KAMATI YA SIASA LUDEWA YARIDHISHWA NA MIRADI

Na. Damian Kunambi, Njombe

Kamati ya Siasa Wilayani Ludewa Mkoani Njombe imekagua na kuridhishwa na mwenendo wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa wito kwa watumishi na wananchi kuhakikisha kuwa wanatunza miradi mbalimbali katika maeneo yao Ili iweze kudumu Kwa muda mrefu na kuweza kuwasaidia.

Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa Barabara ya Mawengi Makonde yenye urefu wa km. 28 na kugharimu kiasi cha Sh. Bil. 1.4 sambamba na utoaji huduma na utunzaji wa miundombinu ya majengo ya kituo cha afya Makonde ambacho ujenzi wake umegharimu kiasi Cha Sh. Mil. 508 na kinahudumia wakazi zaidi ya 17,341 wa Kata hiyo na Kata za jirani Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gervas Ndaki kwa niaba ya mwenyekiti wa Chama hicho Stanley Kolimba amesema kamati hiyo imeridhishwa na hali ya miradi hiyo huku ikitoa maelekezo ya marekebisho madogo madogo ikiwemo upakaji rangi.

Aidha Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Silvanus Thomas amesema amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi huku akiwataka watumishi kujituma kwa moyo na kufanya kazi pasipo manung’uniko yoyote kwani juhudi zao za kazi ndizo pekee zinaweza kuwainua.




Related Posts