Waliochomwa moto Handeni: Ni uhalifu au kisasi?

Tanga/Dar. Mume wa Jonaisi Shao aliyekutwa amefariki dunia pamoja na mwanawe wa kiume na dada wa kazi kwa kuchomwa moto, eneo la msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel, uliopo Kijiji cha Sindeni wilayani Handeni mkoani Tanga, amesimulia mara ya mwisho alipowasiliana naye.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 24, 2024 kuhusu tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema tukio hilo limetokea jana Septemba 23, saa tatu usiku.

Amesema Polisi lilipokea taarifa kuwa ndani ya msitu huo kuna gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 305 EAL linaungua moto na pembeni yake kuna watu wawili wanaungua.

Kamanda amesema askari walifika eneo hilo na kukuta kuna gari ndogo linaungua moto na pembeni yake kukiwa na watu wawili wameungua kwa moto na kufariki.

Bedan Shao enzi za uhai wake.

Mchunguzi amesema baada ya uchunguzi wa awali ilibainika miili iliyokuwa nje ya gari ni ya jinsia ya kike na ndani ya gari kiti cha nyuma ulionekana mwili mwingine ambao umeungua moto hadi kupoteza sura na haijabainika ni wa jinsia gani.

Amesema Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikisha na vyombo vingine vya uchunguzi kubaini walioteketea kwa moto ni kina nani, nini kiliwatokea kabla ya mauti na waliofanya tukio hilo ni watu gani, ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Kamanda amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni, kwa ajili ya uchunguzi.

Msitu wa Korogwe Fuel unamilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Handeni.

Akizungumza na Mwananchi mume wa marehemu, Lameck Shao amesema alikuwa akiwasiliana na mkewe hadi jana (Septemba 23) saa tatu usiku kabla ya mawasiliano kukatika.

“Tuliwasiliana vizuri hadi saa tatu kwamba amefika nyumbani baada ya hapo akawa hapatikani, nilijaribu kutafuta namna ya kupata mawasiliano hadi asubuhi ya leo (Septemba 24) nilipomtuma kijana wa shamba aende pale nyumbani.

“Baada ya kufika, yule kijana hakukuta mtu na alipozungumza na majirani walibaini milango iko wazi. Tulianza kufuatilia ndipo mchana tuliposikia taarifa kwamba kuna watu wameungua kwenye gari,” amesema.

Mbali na Jonaisi amesema wengine waliofariki dunia ni mtoto wao wa mwisho, Bedan Shao na msichana wa kazi.

Awali, ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Johan Shao, amesema ndugu yake amefariki dunia muda mfupi baada ya kuwasili nyumbani kwake Korogwe.

Amesema Jonaisi alitoka Dar es Salaam akielekea Korogwe kujiandaa kwenda mkoani Kilimanjaro kuhudhuria maziko ya baba yao mdogo Charles Shao, katika Kijiji cha Maring’a Kondiki, Mwika.

“Jonaisi alikuwa anafanya kazi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe hivyo alikuwa na makazi Korogwe na Dar es Salaam.”

“Taarifa za msiba zilimfikia akiwa Dar hivyo jana (Septemba 23) jioni akafunga safari kwa ajili ya kuwahi mazishi yanayofanyika kesho (Septemba 25). Wakati wote wa safari alikuwa anawasiliana na mume wake hadi alipofika alimjulisha,” amesema.

“Kwa mujibu wa mumewe mawasiliano yalianza kukosekana baada ya kufika Korogwe, alimtafuta usiku wote wa jana hakufanikiwa kumpata kwenye simu. Alifanya hivyo hadi asubuhi ya leo lakini hakumpata hadi pale alipowasiliana na majirani ambao walimfahamisha kwamba milango ya nyumba iko wazi na hakuna mtu wala gari,” amesema.

Amesema jitihada za kumtafuta ziliendelea hadi mchana ndipo zikaja taarifa kwamba kuna tukio la watu kuchomwa moto kwenye gari.

“Walipofuatilia zaidi ndiyo ikabainika ni yeye Jonaisi na pale nyumbani hakukuwa na dada wa kazi wala mtoto inasemekana ndio hao alikuwa nao kwenye gari,” amesema.

Amesema familia bado haijapata taarifa za kina kuhusu tukio hilo, lakini mume wa marehemu na baadhi ya ndugu wamesafiri kuelekea Korogwe.

Related Posts