Kazi ipo kwa Srelio  | Mwanaspoti

WAKATI Srelio ikiwa katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), kocha msaidizi wa timu hiyo, Miyasi Nyamoko amesema mchezo wao wa mwisho utakaopigwa kesho dhidi ya Mgulani (JKT) ndiyo utakaoamua wacheze nafasi hiyo.

Akizungumza na Mwanasposti katika Uwanja wa Donbosco Oysterbay, Nyamoko alisema kuendelea kushika nafasi ya  nane itategemea na mchezo huo kutokana na namna wakavyozichanga karata zao.

“Tukishinda tukakuwa tumefikisha pointi 44 zitakazotufanya tucheze hatua ya nane bora,” alisema Nyamoko.

Alisema endapo watapoteza mchezo watapata pointi 43 zitakayofanya wazidiwe moja na Mgulani (JKT), na kwamba kuzidiwa huko kutategemea endapo timu hiyo itashinda michezo yote mitano iliyobaki.

Msimamo wa ligi hiyo unaonyesha Mgulani JKT imecheza michezo 25 ikiwa na pointi 34 imebakiwa na michezo mitano ikamilishe 30 ya mzunguko wa pili. Kwa mujibu wa sheria na kanuni za mchezo wa kikapu, inayoshinda itapata pointi mbili na ikifungwa moja.

Wakati huo huo timu ya kikapu ya Tausi Royals imewashangaza wengi baada ya kuifumua Vijana Queens kwa pointi 57-38 katika mchezo wa mchezo wa Ligi ya Kikapu MKoa wa Dar es Salaam (BDL).

Mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wengi na kufanyika katika Uwanja wa Donbosco Oysterbay, uliwaduwaza watazamaji kwa namna Tausi Royals ilivyokuwa ikicheza huku ikiwa na uwiano mzuri wa kukaba na kushambulia, tofauti na Vijana iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kushinda.

Tausi Royals ambayo ni timu ngeni katika ligi hiyo ilianza mchezo katika robo ya kwanza kwa uelewano mzuri, huku ikitumia nguvu kama silaha yake kukabiliana na mastaa wa wapinzani wao.

Mbali ya kutumia nguvu, timu hiyo ilidhibiti pia maeneo ya katikati kwa kuimarisha ulinzi, jambo lililoifanya Vijana kupoteana.

Tangu robo ya kwanza Vijana Queens ilionekana haikuwa kwenye maandalizi mazuri kwani nyota wake walipokonywa mipira mara kwa mara na kuruhusu mashambulizi langoni kwao.

Katika mchezo huo Tausi Royals iliongoza katika robo tatu zote kwa pointi 25-9, 12-10, 8-5, 12-14.

Related Posts