Bibi aliyeuawa kwa kukatwa panga Sengerema azikwa

Buchosa. Sarah Petro (74) aliyeuawa Septemba 22, 2024 kwa kukatwa kwa panga na watu wasiojulikana amezikwa.

Maziko yamefanyika Septemba 24, 2024 nyumbani kwake Kitongoji cha Mizorozoro, Kijiji cha Magulukenda, Kata ya Kalebezo wilayani Sengerema.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 25, 2024, Paul Petro ambaye ni mtoto wa marehemu amesema kifo cha mama yake ni cha kikatili kilichofanywa na watu wasio na huruma.

Ameiomba Serikali kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji hayo wanapatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Petro amesema mama yake hakuwa na ugomvi na mtu yoyote ndani ya Kijiji cha Magulukenda hivyo tukio la mauaji yake linastaajabisha.

“Kama ni mpango wa Mungu basi umetimia,” amesema.

Mkazi wa Kitongoji cha Mzorozoro, Juma Hassan amesema kukatisha uhai wa mwanadamu ni kitendo cha kinyama ambacho hakikubaliki ndani ya jamii.

Amesema wanadamu wanapaswa kuishi na kumcha Mungu.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amesema hadi sasa watu wawili wamekamatwa kwa mahojiano zaidi, akiwamo mtoto wa kike wa marehemu.

Amesema Serikali iko kazini ikifanya uchunguzi juu ya tukio hilo, akiiomba jamii kutulia na kuviacha vyombo vya dola vifanye kazi yake.

Ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha kukamatwa kwa waliotenda kitendo hicho.

Related Posts