BAADA ya kusemekana Simba Queens ipo kwenye mazungumzo na makocha kutoka nchi tano tofauti akitajwa Birhanu Gizaw, Kocha wa Ethiopia ni kama dili limegeuka na sasa wamemalizana na kumgtambulisha Yussif Basigi raia wa Ghana aliyekuwa akiinoa Hasaacas Ladies ya nchini humo.
Awali ilielezwa kuna uwezekano mkubwa wa Gizaw kuja kuwa mrithi wa aliyekuwa kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda lakini sasa Simba ni kama imempotezea na kumgeukia Basigi iliyemtambulisha mchana huu.
Inaelezwa Simba imeshindwana na Muethiopia kwenye mambo ya kimaslahi ambayo alitaka fedha kubwa ilihali timu hiyo haina uwezo wa kumpatia isitoshe wekundu hao wa Msimbazi walihitaji kocha mwenye uzoefu Ligi ya Mabingwa Afrika wakati ambao Gizaw amejizolea umaarufu ukanda wa CECAFA akibeba taji hilo wiki chache zilizopita.
Baada ya kushindwana inaelezwa Simba ikamrudia Mghana waliyepatana kwenye maslahi na ni kocha mwenye CV kubwa CAF.
Kocha huyo wa timu ya taifa ya Ghana inaelezwa ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza baada ya kumaliza mkataba na Hasaacas ambayo tayari ameipa mkono wa kwaheri.
Chanzo kililiambia Mwanaspoti kuwa viongozi wa timu hiyo wamevutiwa zaidi na Basigi ambaye inaonekana wanaweza kufanya kazi naye baada ya makubaliano ya awali.
“Ilibaki kidogo yule kocha wa Ethiopia aje kuifundisha Simba lakini viongozi wamepiga hesabu wanaona haziendi hivyo wakamtafuta Mghana ambaye amevutiwa sana kuja kufundisha Tanzania na kikubwa ni wasifu alionao,” kilisema chanzo hiko.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Simba, Seleman Makanya kuhusu ishu ya usajili alisema bado timu haijatoa ufafanuzi juu ya kocha mpya.
“Mimi mwenyewe nashangaa kusikia hilo lakini uongozi wa timu bado haujatoa taarifa kamili tuwasubiri wao kama kweli ishu ya kocha ipo,” alisema Makanya.
Kocha huyo mwenye Leseni A ya ukocha alijiunga na Hasaacas mwaka 2013 akiweka rekodi ya kocha aliyedumu muda mrefu zaidi kwenye kikosi hicho ambacho amekipa mafanikio mbalimbali.
Ameipatia timu hiyo ubingwa wa Ligi ya Ghana mara nne akichukua miaka mitatu mfululizo msimu wa 2012-13, 2013–14, 2014–15 na 2020–21.
Kimataifa aliisaidia timu hiyo kufuzu Klabu bingwa kwa Wanawake mwaka 2021 ukanda wa WAFU ambapo baadae aliibuka mshindi wa pili baada ya kutolewa na Mamelodi Sundown kwenye fainali hiyo iliyochezwa nchini Misri kwa jumla ya mabao 2-0.
Kwenye timu za taifa za wasichana mwaka 2015 aliisaidia Black Princess kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake Under-20, Ufaransa 2018, Mashindano ya Michezo ya Afrika 2015, Congo Brazzaville.