Tanga. Jumla ya wafungwa 746 mkoani hapa wamenufaika na msamaha Bodi ya Parole, wakiwamo 375 waliopata msamaha wa Rais baada ya kutathiminiwa na wengine 371 wakimaliza vifungo vyao kwa kusimamiwa na bodi hiyo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian wakati akizindua Bodi ya Parole ya mkoa huo ofisini kwake jana Septemba 24, 2024 na kusema kuwa wajumbe wa bodi hiyo wanatakiwa kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa weledi na wafungwa wananufaika na uwepo wao.
Amesema kwa utaratibu ulivyo hata kama mfungwa husika amepewa nafasi ya kuwa huru ila akiwa uraiani kwenye jamii akionyesha tabia mbaya, sheria inaruhusu kurudishwa tena gerezani, hivyo kuwataka wanaopata msamaha kwenda kuwa mfano mzuri katika jamii.
“Ninawaomba wale walionufaika na utaratibu wa Parole wawe mabalozi wazuri huko walipo na ni matumaini yangu jamii inayowazunguka itawaona kama mfano bora na kwamba hawatafanya tena vitendo vibaya,” amesema Balozi Burian.
Mwenyekiti wa bodi hiyo mkoani hapa, Padre Silvester Ludovick amesema wafungwa wanaofaidika na bodi ni wale ambao wameonyesha kujutia makosa yao na waliotumia theluthi ya kifungo chao.
Pia mfungwa husika hutakiwa kuzingatia masharti ambayo amepewa na Parole, kuyafuata kikamilifu na mamlaka ikijiridhisha basi anaweza kuingizwa kwenye msamaha huo.
Katibu wa bodi hiyo ambaye ni Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Hudson Masawe ameongeza kuwa utaratibu huo unasaidia magereza kupunguza wingi wa wafungwa, lakini baadhi kupata elimu na kuwa mfano kwa jamii.
Mjumbe wa bodi hiyo Monica Kinala ameiomba Serikali kuziwezesha bodi hizo, kwenda kutoa elimu kupitia vyombo vya habari ili wananchi wajue uwepo wao na wananufaika nayo vipi, ili iweze kuwasaidia wananchi waliopo magereza.
Wajumbe wa bodi za Parole za mkoa huteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo kwa mkoa wa Tanga hiyo ni bodi ya 46 kuzinduliwa tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo mwaka 1994.