MWAMUZI wa kati, Hery Sasii ndiye atakayesimamia mchezo wa kuvutia na kusisimua wa Ligi Kuu Bara wa ‘Mzizima Dabi’ kati ya wenyeji Azam FC dhidi ya Simba utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa New Complex Amaan visiwani Zanzibar saa 2:30 usiku.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa zinaeleza kwamba, Sasii ndiye mwamuzi wa kati aliyependekezwa na kamati ya waamuzi kwa ajili ya kuzitafsiri sheria 17 za mpira wa migumu, wakati miamba hiyo itakapokuwa inapambana kesho Alhamisi.
“Mjadala ni mkubwa kwenye kamati kwa sababu kila mtu amekuwa na mapendekezo yake ya kuchagua mwamuzi anayeona ataendana na kasi ya mchezo huo, ila hadi sasa kura nyingi zimeonekana kumuangukia, Hery Sasii,” alisema mmoja wa mtoa taarifa.
Mtoa taarifa huyo ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake aliongeza, waamuzi wa pembeni waliopendekezwa ni Mohamed Mkono wa Tanga na Zawadi Yusuph wa Dar es Salaam huku Amina Kyando kutoka Morogoro akiwa ni mwamuzi wa akiba (fourth official).
Mchezo wa mwisho kwa timu hizo kukutana uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar ulikuwa ni wa fainali ya Kombe la Muungano Aprili 27, mwaka huu na Simba ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Babacar Sarr.
Katika Ligi Kuu Bara, mchezo wa mwisho kwa miamba hiyo kukutana ulipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 9, mwaka huu ambapo Simba iliibuka kidedea kwa mabao 3-0, yaliyofungwa na Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na David Kameta ‘Duchu’.
Azam FC itakutana na Simba chini ya kocha mpya, Fadlu Davids ambaye ameshinda michezo yote miwili ya Ligi Kuu Bara hadi sasa aliyoiongoza baada ya kuifunga Tabora United kwa mabao 3-0, Agosti 18, kisha kuichapa Fountain Gate 4-0, Agosti 25.
Kwa upande wa Azam ambayo pia iko chini ya kocha mpya Mmorocco, Rachid Taoussi, ilianza Ligi Kuu Bara kwa suluhu mbili mfululizo dhidi JKT Tanzania na Pamba kisha kuzinduka kwa KMC kwa kuichapa mabao 4-0, na kuifunga Coastal Union bao 1-0.s