JKT yatangaza nafasi za kujitolea, utaratibu huu hapa

Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT ya kujitolea kwa mwaka 2024, ambapo usajili utaanza Oktoba Mosi, 2024.

Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Kanali Juma  Mrai ameyasema hayo leo Jumatano, Septemba 25, 2024  alipokuwa akitangaza  wito wa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea mwaka 2024  uliotolewa na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele.

Amesema utaratibu wa kuomba na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unaratibiwa na ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya ambako mwombaji anaishi.

Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Kanali Juma  Mrai akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Amesema Meja Jenerali Mabele anawataarifu vijana wote wa Tanzania Bara na Zanzibar kuwapo nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2024.

“Usajili wa vijana wa kujiunga na mafunzo hayo utaanza Oktoba 1 mwaka huu kwa mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani,” amesema.

Amesema vijana watakaoteuliwa watatakiwa kuripoti kwenye makambi ya JKT kuanzia Novemba Mosi hadi 3, 2024.

Aidha, Kanali Mrai amewataarifu vijana watakaopata fursa hiyo kuwa JKT haitoi ajira, pia haihusiki kuwatafutia ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama na mashirika mbalimbali ya Serikali na yasiyo ya kiserikali.

Amesema kinachofanyika ni kutoa mafunzo ambayo yatawasaidia vijana kujiajiri wenyewe mara baada ya kumaliza mkataba wao na JKT.

“Sifa za mwombaji na maelekezo ya vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo yanapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz,” amesema.

Kanali Mrai amesema Meja Janerali Mabele anawakaribisha vijana wote watakaopata fursa hivyo kuja kujiunga na vijana wenzao, ili kujengewa uzalendo, umoja wa kitaifa, ukakamavu, kufundishwa stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kuitumikia Taifa lao.

Nafasi hizi za kujiunga na mafunzo ya JKT ni bure na haziuzwi na kwa ni kwa vijana wote wa Kitanzania watakaokidhi vigezo vilivyoainishwa.

“JKT halitahusika na kwa namna yoyote ile pindi mzazi au malezi atakapotapeliwa kwa kutoa fedha, Makao Makuu ya JKT hakuna nafasi ya vijana kujiunga na mafunzo ya JKT nafasi zote zimepelekwa mikoani ambazo zitagawanywa katika wilaya mbalimbali za mikoa husika.”

Mmoja wa wakazi wa jijini Dodoma, Juma Jumanne amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwapatia vijana ujuzi wa shughuli mbalimbali ambao watautumia kujiajiri.

“Wapo ambao walipitia mafunzo haya wameanzisha shughuli zao na wametoka kimaisha. Inatakiwa kijana ajiongeze baada ya kuhitimu mafunzo,” amesema.

Related Posts