Hii hapa sababu, chimbuko na maana ya Wangoni kugaragara

Songea. Ingawa kugaagaa  au kugaragara wengine wanakuhusisha na mitazamo hasi, kwa kabila la Wangoni ni utaratibu unaobeba tafsiri lukuki zinazoashiria heshima na adabu.

Mtindo wa kugaragara chini kwa mujibu wa Wangoni, ni tafsiri halisi ya kiwango cha mwisho cha kushukuru, kuomba radhi na kufurahi.

Hata hivyo, kitendo cha kugaragara kimeibua mijadala mitandaoni baada ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama kufanya hivyo jana Jumanne, Septemba 24, 2024 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Jenista ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho, aligaragara akiashiria kumshukuru Rais Samia kwa kuwezesha utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo.

Kitendo hicho kimeibua mijadala mitandaoni sanjari na picha yake kusambaa ikimwonyesha anavyo garagara.

Mwananchi limezungumza na watu mbalimbali kujua asili ya utamaduni huo na una maanisha nini.

Chimbuko la kugaragara au kugaagaa

Akizungumzia hilo, Kiongozi wa kimila wa kabila la Wangoni, Chifu Inkas Songea Mbano, anasema chimbuko la utamaduni huo ni enzi za uasisi wa kabila la kingoni.

Anasema wazee walioasisi tamaduni zote za kabila hilo, ndiyo waliokuwa wakitumia mtindo huo, kuashiria mambo mbalimbali, ikiwemo kushukuru, kuomba radhi na kuonyesha kiwango cha mwisho cha furaha.

Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya akilala chini ikiwa ni ishara ya shukrani na furaha kwa mujibu wa mila za wangoni na wamatengo wakati alipokabidhiwa ufunguo wa gari la kubebea wagonjwa na Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma. Picha na Mtandao

“Wazee walifanya hivi, utamaduni unaishi nasi tunapaswa kufanya isipokuwa vijana wengi wa sasa hawaelewi haya mambo ndiyo maana wanaona ajabu,” anasema.

Ni kushukuru, kuomba radhi na kufurahi

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, unapoona mtu ameongea au kutenda jambo lililokufurahisha, inakupasa kugaagaa chini, ukiashiria kushukuru.

Anasema kugaagaa huko, hakuishii kuakisi shukurani pekee, bali ni ishara ya kuomba kilichofanywa lifanywe tena kwako au katika eneo lingine kwa masilahi ya wengine.

“Ni sawa na kusema tunakushukuru umetusaidia, tunaomba tena utusaidie kama hivi na usaidie wengine katika maeneo mengine,” anafafanua.

Lakini Songea, anaeleza kugaagaa hakufanywi kuashiria kushukuru pekee, bali hufanyika pia nyakati za kuomba msamaha au radhi.

Isipokuwa wakati wa kuomba radhi, anasema pamoja na kugaagaa chini, aliyekosea anapaswa kumshika miguu aliyemkosea.

“Hapo mkosaji atagaagaa chini kisha kumshika miguu aliyemkosea na kutamka kwamba nimekosa, hiyo inamaanisha mkosaji hatarudia kosa lile,” anasema.

Kwa mujibu wa chifu huyo, hata sasa utamaduni huo unatumika kwa baadhi ya wenza, akisema kabla mwanaume hajachukua uamuzi mgumu anapokosewa au wanapotofautiana, mwenza wake hugaagaa kuomba radhi.

“Kwa kawaida mtu anapogaagaa kama ni kuomba msamaha lazima asamehewe, kama ni kushukuru lazima aeleweke. Maana ni kiwango cha mwisho cha furaha, heshima na msamaha kwa Wangoni,” anasema.

Hata hivyo, anasisitiza si kila shukurani, msamaha na ombi linaombwa kwa kugaagaa, hatua hiyo inamaanisha kiwango cha mwisho cha jambo.

Ni wanawake ndiyo hupaswa kugaagaa

Songea, anasema aghalabu wanawake ndiyo wanaoonyesha ishara hiyo kwenye mambo mbalimbali, kwa upande wa wanaume kuna mtindo tofauti.

Anasema wanaume wanaposhukuru, wanapaswa kupiga goti na kutamka shukurani zao, lakini wanatakiwa kufanya hivyo wanapoomba radhi pia.

Kwa mujibu wa Songea , mwanaume anapoomba radhi pamoja na kupiga goti atapaswa kumshika miguu aliyemkosea.

“Hata kwa mkewe mwanaume anapokosea anatakiwa kupiga goti na kumshika miguu kama ishara ya kuomba msamaha. Hadi sasa baadhi tunafanya,” anasema.

Songea, anasema kitendo hicho pia, hufanywa katika matukio mbalimbali muhimu hasa kwenye harusi.

Katika harusi, anasema wakwe na ndugu wa mke kwa tamaduni za kingoni, wanapaswa kugaagaa kuashiria furaha na shukurani.

Anasema wanaohusisha kitendo hicho na kujipendekeza wanakosea, na inawezekana hawajui uhalisia wa kitendo hicho kwa Wangoni.

“Kwa wazee wa kingoni unaomkosea unapiga goti chini na kuomba msamaha, hata kama alipanga adhabu gani atakusamehe. Hizi ni tamaduni zetu sio kujipendekeza.

“Kwanza mwanamke anayegaagaa anaonyesha ameheshimika, amestaarabika na ana adabu, vivyo hivyo kwa mwanaume anayepiga goti,” anasisitiza.

Kutokana na wimbi la kuingia kwa tamaduni za kigeni Songea, anasema mtindo huo wa kugaagaa unatekelezwa mara chache na wengi hutafsiri vibaya.

“Tamaduni zetu zinatoweka sasa hivi mtu akigaagaa anaonekana mshamba au atatafsiriwa kwa namna yoyote mbaya. Ni jambo baya sana, tunapaswa tuishi kwa kufuata tamaduni zetu,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza kabila hilo linalenga kuenzi utamaduni huo na nyingine nyingi hasa baada ya Serikali kupitisha baadhi ya sheria zinazowapa machifu hadhi ya kuyatekeleza hayo.

Mkazi wa Songea, Theodosia Thomas anasema ameyashuhudia hayo kwa wazazi wake lakini yeye hakuwahi kufanya utamaduni huo.

“Nimeolewa na mume ambaye si mgoni nikimfanyia hataelewa. Lakini niliwaona wazazi wangu wakifanya hivyo hasa mama,” anasema.

Mbano Nichorous anasema ni wachache waliolelewa katika tamaduni hizo kwa sasa, wengi wanaishi kisasa.

“Kwa sasa wamebaki wachache sana. Ukimwona mwanamke au mwanaume ana utamaduni huo, ujue hapo umepata mwenza sahihi, kama ni ndoa itadumu kwa sababu ndani ya nyumba kunakuwa na adabu,” anasema.

Related Posts