Mbinga. Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya Serikali kufanya kila juhudi za kuwawekea mazingira mazuri wakulima, wenyewe pia wanapaswa kubadilika.
Amesema licha ya Serikali kuweka utaratibu wa wakulima kuuza mahindi kwa bei nzuri kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), baadhi wanauza kwa walanguzi.
Rais Samia amesema hayo leo, Septemba 25, 2024 aliposimama kuzungumza na wananchi wa Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.
“Serikali inatamka vizuri na imejitahidi kila inapoona kuna changamoto za wakulima inazitatua, lakini wakulima wenyewe nanyi mnapaswa kubadilika,” amesema.
Amesema sababu ya kuweka vituo vya NFRA katika maeneo walipo wakulima ni kuhakikisha wanapata masoko yatakayowafaidisha.
Rais Samia amesema baadhi ya wakulima wanakubali kuuza mazao kwa walanguzi ambao mara nyingi hununua kwa bei ya chini zaidi.
“Tumefanya hivyo ili mpate faida ya shughuli za kilimo, hatutaki baadaye mkose fedha za kununua mbolea,” amesema.
Amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinasimamia bei ya Serikali ya mahindi ili wakulima wanufaike.
Katika hatua nyingine, akizindua jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Mbinga, amesema dhamira ya Serikali kujenga jengo hilo ni kuweka mazingira mazuri kwa maofisa wanaotumikia wananchi.
Amesema ubora wa jengo hilo unapaswa ufanane na ubora wa huduma zitakazotolewa kwa wananchi.
Amewataka watendaji kuhakikisha wanaweka nguvu katika kusimamia miradi ili yanayowakera wananchi yasiwepo.
“Sisi ni watumishi kwa wananchi na si watawala kwa wananchi na ndiyo maana Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali,” amesema.
Awali, akijibu baadhi ya changamoto zilizoibuliwa na Mbunge wa Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga kuhusu zikiwamo za mauzo ya kahawa, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imeanza mchakato wa kubadilisha mfumo wa uuzaji wa zao hilo ili kuepusha makato kwa wakulima.
Ameeleza mfumo huo utawezesha wakulima kupokea fedha moja kwa moja kutoka kwa chama kikuu cha ushirika badala ya kupitia michakato mbalimbali.
Bashe amesema mfumo uliopo sasa una michakato mingi, ambayo pamoja na fedha kupitia kwenye vyama vikuu vya ushirika, pia hupita katika chama cha msingi cha ushirika.
“Huu mchakato ni mrefu hatutaki uendelee, tunabadili mfumo na nimeshaandika waraka. Mfumo huu mpya tumeshautumia Lindi kwenye korosho na tutakwenda kuutumia kwenye kahawa.”
“Ule utaratibu wa vyama vya ushirika kwenda kukopa fedha benki kwa majina ya wakulima kisha vinalipa malipo ya awali kwa wakulima, visubiri malipo zaidi, utakwenda kukoma,” amesema.
Hata hivyo, amewahakikishia wakulima kuwa vituo vya NFRA kwa ajili ya kununua mahindi havitafungwa hadi vinunue yote.
Amesema kitajengwa kituo cha zana za kilimo kwa ajili ya kuhakikisha wakulima wanalimiwa mashamba yao kwa Sh40,000 badala ya Sh80,000 za sasa.