Makinda azungumzia uadilifu wa Sokoine, akitaka jamii kuacha unafiki

Dar es Salaam. Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, kujizatiti na kuacha unafiki, ili kumuenzi waziri mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine ambaye ametimiza miaka 40 tangu alipofariki dunia.

Sokoine, mmoja wa wanasiasa walioacha alama hasa katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi katika uongozi wake, alifariki dunia Aprili 12, 1984 kwa ajali ya gari eneo la Dakawa wilayani Mvomero, mkoani Morogoro akitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Makinda aliyewahi kuwa mbunge wa Njombe Kusini, ameeleza hayo leo Jumatano Septemba 25, 2024 wakati wa mahojiano maalumu kuhusu namna anavyomfahamu hayati Sokoine waliyefanya kazi pamoja.

Mahojiano hayo yaliandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi wa kitabu cha hayati Sokoine kuhusu maisha na uongozi wake kitakachozinduliwa Septemba 30, 2024.

“Enzi za uhai wa Sokoine alitufundisha uaminifu na ukweli, hakuwa mnafiki kama umefanya kazi vizuri anakusifia, tuache unafiki na kujipendekeza. Kazi zetu zitatubeba, kikubwa tuwe na matendo mema katika utekelezaji wa majukumu yetu.”

“Pia, Sokoine alifanya kazi kwa bidii na alikuwa mfuatiliaji wa shughuli zote za Serikali ndiyo maana alipendwa na wananchi wakiwamo wa hali ya chini,” amesema.

Makinda amesema Februari 25, 1983 akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu aliwahi kufanya kazi kwa mwaka mmoja na hayati Sokoine akiwa waziri mkuu akieleza alikuwa mstari wa mbele kukabiliana na wahujumu uchumi.

“Kutokana na mapambano haya makubwa wananchi wa kawaida walimpenda kwa sababu alijali watu ndiyo maana alipokwenda kwake (Monduli) Wamasai waliona gari lake ni la kwao,” amesema.

Amesema hakuwa mpenzi wa kupokea zawadi, akitoa mfano kuna waziri mmoja alimpelekea ng’ombe kama zawadi hakukubali, badala yake alimuuliza thamani kisha akamrejeshea fedha zake.

“Hakuweza kuchukua kitu cha mtu hata kidogo, lakini alikuwa mtu anayependa kazi muda wote sijui alikuwa analala saa ngapi? alipenda ibada kwa mwaka alikuwa anakesha mara tatu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph,” amesema.

Amesema vijana kuingia katika nafasi za uongozi si jambo baya lakini waondokane na fikra kwamba, nafasi hizo ni za fursa bali wajikite katika kuwahudumia Watanzania.

“Vijana kuingia kwenye nafasi ni lazima tusiliache hili gap (nafasi) lakini wawe na fikra za kuwatumikia Watanzania ili kufika mbali, lakini kuchunga midomo na kuacha kusema ovyo,” amesema.

Balozi Ali Mchumo aliyefanya kazi na hayati Sokoine amesema mwaka 1975 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo walifanya kazi pamoja katika baraza la mawaziri.

“Alivyoteuliwa uwaziri mkuu, Sokoine alisema ukiteuliwa kushika nafasi yoyote ukiaminiwa na wewe jiamini, kauli hii hadi sasa sijaisahau,” amesema.

Amesema katika kipindi cha mwaka 1977 hadi 1979 alibadilishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati wa vita ya Kagera.

“Wakati huo Sokoine alikuwa mwenyekiti wa kamati ya mawaziri wa vita, ilikuwa kila siku tunakutana asubuhi. Kuna siku alinipigia simu mimi na Jackson Makweta (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati huo) akitutaka twende Kagera.

“Asubuhi tukaondoka na Makweta kwenda Kagera, alitupa maelekezo tuanzie Morogoro hadi Kagera kuhamasisha wakuu wa mikoa kuandaa askari wa Jeshi la Akiba kwa ajili ya vita,” amesema.

Balozi Mchumo aliyewahi kuwa mbunge wa Temeke mkoani Dar es Salaam, amesema pamoja na Makweta walitekeleza jukumu hilo na baada ya kurejea Sokoine alitaka ripori ya kazi aliyowapa.

“Tuliulizwa maswali ya msingi na muhimu, Sokoine alituuliza hili mlisema au lile? Alikuwa mtu wa kutaka taarifa za kina si za juujuu,” amesema.

Kitabu cha maisha ya hayati kinachoitwa ‘Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake’ kinatarajiwa kuzinduliwa Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Septemba 30, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan.

Wengine watakaohudhuria ni pamoja na viongozi wakuu, viongozi waandamizi kutoka kwenye sekta za umma na binafsi, viongozi wastaafu, mabalozi, na wawakilishi wa washirika wa maendeleo, taasisi za elimu ya juu, na asasi za kiraia.

Kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Uongozi na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kinaangazia safari yake, kuanzia makuzi yake katika jamii ya Kimasai, hadi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwemo uwaziri mkuu wa Tanzania. Kitachangia kukuza historia ya Tanzania na Bara la Afrika.

Related Posts