Pemba. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Ashatu Kijaji amewataka waratibu na wasimamizi wa miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Pia amewaagiza kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Dk Kijaji ametoa kauli hiyo leo Septemba 25, 2024 kwenye ziara yake ya kikazi kukagua miradi inayosimamiwa na kutekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kisiwani Pemba.
Miongoni mwa miradi hiyo ni wa kuimarisha miundombinu ya Fukwe, Sipwese, Mkoa wa Kusini Pemba na mradi wa jamii wa ujenzi wa ngazi na ukuta katika Shehia ya Kizimbani, Kaskazini Pemba.
Amesema kila mmoja anapaswa kusimamia vyema eneo alilopewa ili kukamilisha kwa wakati miradi na wananchi waweze kunufaika nayo.
“Viongozi wetu wanatupenda ndiyo maana leo nimetumwa hapa kuangalia kinachoendelea, hivyo nitoe wito kwa wasimamizi wa miradi kuongeza kasi ya ujenzi na itakapokamilika kila mmoja ana wajibu wa kuilinda,” amesema.
Dk Kijaji amesema eneo la Sipwese ambalo linajengwa tuta kuzuia maji ya bahari kumekuwa na mmomonyoko ambao umeanza kuleta athari katika baadhi ya maeneo kwa kusababisha uharibifu wa barabara, majengo, makazi ya watu na madaraja, hivyo kuilazimu Serikali kutumia gharama kubwa kufanya ukarabati huo.
Katika mradi wa utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika Shehia ya Kizimbani, Dk Kijaji amesema unalenga kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu.
Pia kusaidia kujenga rasilimali watu hasa watoto kwa kuwapa elimu, huduma za afya na lishe bora.
Mkuu wa Wilaya ya Wete, Mkoa Kaskazini Pemba, Dk Hamad Omar Bakari amesema walengwa wa Shehia ya Kizimbani pia wamebahatika kupata mafunzo maalumu ya siku saba ya ruzuku ya uzalishaji na kuandaa mipango rahisi ya biashara.
Baadhi ya wananchi katika maeneo hayo akiwemo Ashura Kombo ameeleza wanavyopata changamoto kutokana na maji kuingia kwenye makazi yao, lakini baada ya kujengewa ukuta kadhia hiyo itapungua.
“Hali ya hapa ni hatari maji yanapanda kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, lakini ngazi na ukuta umesaidia kupunguza athari zinazojitokeza,” amesema.
Mradi wa daraja la kupandia na kushuka lenye urefu wa mita 82 limewawezesha wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo kufika kwa urahisi katika mashamba yao.