Idadi ya watoto wasiokwenda shule ni jumla ya milioni 250 kote duniani, kulingana na takwimu za 2023 za shirika la UNESCO. Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inachukua karibu asilimia thelathini ya watoto wote ambao hawajaenda shule kote ulimwenguni, na idadi hiyo inaendelea kuongezeka.
Migogoro ya kivita imesambaratisha jamii na kusababisha watu wengi kuyahama makazi yao. Dk. Ibrahim Baba Shatambaya, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Usmanu Danfodiyo Sokoto, Nigeria, aliiambia DW kwamba “Changamoto kuu wanayokabiliana nayo wakati huo haihusiani na kupata elimu, bali jinsi ya kupata mahitaji ya kimsingi ya kuishi – chakula, maji, na huduma za matibabu.”
Kwa upande wake Hassane Hamadou, mkurugenzi wa kanda wa Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) amesema kuna pia suala la vurugu zinazoathiri shule moja kwa moja. Amesema elimu imezingirwa katika eneo Afrika Magharibi na Kati huku shule zikilengwa kimakusudi na kunyimwa elimu kimfumo kwa sababu ya mzozo pia ni janga.
Nchi kama Nigeria, Cameroon, Burkina Faso, Mali, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinabeba mzigo mkubwa wa mgogoro huu huku shule zikishambuliwa mara kwa mara na makundi yenye silaha.
Soma: Shikika la KidsRight: Haki za watoto zazidi kukiukwa duniani
Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, inakabiliwa na mzozo mkubwa wa elimu. Zaidi ya watoto milioni 15.23 hawako shuleni, kulingana na shiorika la UNESCO. Tatizo hilo kwa kiasi kikubwa linaathiri eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, ambalo limezingirwa na wanamgambo wa Boko Haram na mgogoro wa utekaji nyara katika miongo kadhaa iliyopita.
Sababu za kuenea kwa migogoro katika kanda hilo la Afrika magharibi na Afrika ya kati ni nyingi, alisema Michael Ndimancho, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Douala nchini Cameroon, akitaja mfano wa uasi wa Boko Haram.
“Unapoangalia nchi kama Nigeria na Cameroon unakuta kwamba kuna masuala mengi ya kihistoria yanayofanana, kwa mfano uasi wa Boko Haram. Na katika Afrika Magharibi na Kati, pia kuna tatizo la mipaka sio tu ni mikubwa bali iko wazi, haidhibitiwi.
Kwa upande wake, Dk. Ibrahim Shatambaya, amesema tatizo ni suala la utawala zaidi nchini Nigeria katika ngazi za mitaa, jimbo na serikali ya shirikisho.
Hali ni kama hiyo ya Nigeria kwenye mikoa ya Cameroon inayozungumza kingereza. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya watoto 700,000 mwaka 2021, na 855,000 mwaka 2019 hawakuwa shuleni Kaskazini-Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon, ambapo makundi yenye silaha ya kujitenga yalilenga shule.
Soma: UN yarekodi idadi kubwa ya ukiukaji dhidi ya watoto katika maeneo ya migogoro
Watoto wengi katika mikoa hii ya nchi wamekuwa nje ya shule kwa miaka mingi. Valentine Tameh, mwalimu wa Cameroon na mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi, anasema hali inazidi kuwa mbaya hivi sasa.
Kulingana na wataalamu, madhara ya muda mrefu ya mamilioni ya watoto kunyimwa fursa ya kupata elimu tayari yanaonekana katika bara zima la Afrika. Juhudi za kushughulikia mzozo huu wa elimu katika bara zima zimekuwa hazifaulu. Wakati mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa yametoa baadhi ya misaada, wakosoaji wanasema juhudi zao hazitoshi kutatua chanzo cha machafuko. Uharibifu umeenea, na bila hatua za haraka, kizazi kizima kinaweza kupotea kwa vurugu, umaskini na ukosefu wa fursa.