Kagera yavimbia Ligi Kuu, beki akituma salamu

BAADA ya kuonja ushindi wa kwanza Ligi Kuu, Kagera Sugar imetamba kuwa imepata mwanga mpya na sasa iko tayari kwa mwendelezo wa michuano hiyo ikiwavimbia Fountain Gate.

Kagera Sugar haikuwa na mwanzo mzuri ilipocheza mechi tatu mfululizo bila kuonja ushindi wala sare kabla ya mchezo uliopita dhidi ya Ken Gold kutakata kwa mabao 2-0 na kuamsha upya nguvu.

Timu hiyo yenye miaka 20 Ligi Kuu, kwa sasa inajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa Septemba 27 katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara.

Timu hizo zinakutana ikiwa wenyeji wanakumbuka ushindi walioupata ugenini dhidi ya Tabora United, huku rekodi ikionesha wawili hao kwenye mechi 10 walizokutana,Kagera Sugar ameshinda minne kwa mitatu na sare tatu.

Beki wa timu hiyo, Chilo Mkama amesema baada ya msoto kwa sasa wamejipata na wanahitaji kuendeleza heshima yao kwa kila mchezo kuhakikisha wanapata pointi tatu.

Amekiri ligi kuanza kwa ugumu, akieleza kuwa ushindi walioupata umewapa ari na kujiamini na kwamba nguvu zote zinawaza mchezo ujao na Fountain Gate kuhakikisha wanashinda ili kujiweka pazuri.

“Hatukuwa na mwanzo mzuri lakini ushindi wa juzi umetupa kujiamini na tunaenda kupambana dhidi ya Fountain Gate kuhakikisha tunalinda ushindi ili kujiweka pazuri,” amesema beki huyo.

Ameongeza kuwa pamoja na matumaini makubwa waliyonayo, lakini wanafahamu mechi itakuwa ngumu kutokana na wapinzani walivyo na ushindani, akieleza kuwa kiu yao ni pointi tatu.

Related Posts