Dodoma. Idadi ya vijana katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, inaonyesha wako milioni 21.3 kati ya watu milioni 61.
Hii inaonyesha umuhimu wa vijana kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa.
Takwimu hizo za sensa zinatoa taswira kuwa zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu nchini ni vijana.
Vijana wanaweza kuleta mawazo mapya, ubunifu na mikakati mipya ya kusukuma mbele maendeleo katika jamii zao.
Wanapokosa ushiriki katika nafasi za uongozi, wanakosa fursa na kuathiri sera na uamuzi muhimu unaohusu hatima yao.
Ili kukabiliana na changamoto inayowakwaza vijana kugombea uongozi, vyama vya siasa vinashauriwa kuwa na mipango maalumu ya kuwasaidia vijana kifedha nyakati za uchaguzi.
Kwa kufanya hivyo, vijana wengi wataweza kugombea na kuongeza uwakilishi wao katika nafasi za uongozi.
Hata hivyo, changamoto ya rasilimali fedha inahitaji ufumbuzi wa muda mrefu zaidi.
Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuwekeza katika programu za kuwawezesha vijana kiuchumi ili wamudu gharama za kugombea nafasi za uongozi bila kutegemea msaada mkubwa wa kifedha.
Pia, ni muhimu kujenga utamaduni wa kuchangishana ndani ya jamii kwa ajili ya kusaidia vijana wanaotaka kugombea nafasi za uongozi.
Mbali na changamoto za uhamasishaji fedha, kuna haja ya kutoa elimu ya kutosha kwa vijana kuhusu nafasi na majukumu yao katika uongozi.
Elimu hii inaweza kutolewa kupitia shule, vyuo na taasisi mbalimbali za kijamii.
Vijana wanahitaji kuelewa kwamba, kushiriki katika siasa si tu kwa ajili ya kupiga kura, bali pia wana nafasi ya kugombea na kushika nafasi za uongozi.
Wanapaswa kuelewa kuw, wana fursa ya kuleta mabadiliko katika jamii zao kwa kushiriki moja kwa moja katika uongozi.
Hii itasaidia kuondoa dhana kwamba, siasa ni kwa ajili ya watu wazima pekee au vijana hawana uwezo wa kuongoza.
Elimu ya uraia inapaswa kuwa sehemu ya mtalaa wa shule ili kuwafundisha vijana kuhusu haki zao za kisiasa na kuwahamasisha kushiriki katika mchakato wa kuongoza nchi yao.
Kwa upande mwingine, vijana wenyewe wanapaswa kuchukua hatua ya kwanza.
Wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za mtaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
Wao ndio kundi lenye nguvu na idadi kubwa, hivyo wana uwezo wa kuleta mabadiliko katika uongozi wa nchi.
Wanapaswa kutumia fursa walizonazo kuhakikisha wanakuwa sehemu ya uamuzi unaohusu mustakabali wa nchi yao.
Vijana ni nguvukazi muhimu kwa Taifa lolote. Kwa idadi yao kubwa, wana nafasi ya kuwa wachezaji wakuu katika kukuza uchumi wa nchi.
Vijana wakiwa na uongozi kwenye ngazi za mtaa, kijiji au kitongoji, wanaweza kutumia nafasi hiyo kuanzisha na kuendeleza miradi inayolenga kukuza uchumi wa jamii, hivyo kusaidia maendeleo ya Taifa kwa jumla.
Kwenye ngazi za mtaa, kijiji na kitongoji, vijana wanaweza kusimamia miradi ya kiuchumi kama vikundi vya uzalishaji mali, biashara ndogo ndogo, kilimo na ufugaji.
Kwa mfano, miradi ya kilimo inaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula, hivyo kupunguza tatizo la njaa na kukuza pato la Taifa.
Pia, miradi ya biashara ndogo ndogo inaweza kusaidia kuongeza ajira kwa vijana wenzao na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa jumla.
Ushiriki wa vijana katika uongozi unaweza kuwa kichocheo cha kuleta maendeleo endelevu kwa sababu wanaweza kutumia ubunifu wao, maarifa na teknolojia ili kuboresha uchumi wa jamii zao.
Kuimarisha amani, utulivu
Uchaguzi wa Serikali za mitaa unalenga ngazi zinazohusisha maisha ya kila siku ya wananchi.
Uongozi katika ngazi hizi una nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa, amani na utulivu vinadumishwa.
Vijana wanaposhiriki katika kugombea na kushika nafasi za uongozi kwenye ngazi za kijiji, mtaa na kitongoji, wanaweza kusaidia kutatua migogoro inayoweza kuibuka katika jamii zao kwa njia za amani na maelewano.
Kwa kuwa vijana mara nyingi ndio wahusika wakuu katika migogoro ya kijamii na kisiasa, wanaposhika nafasi za uongozi wanaweza kuwa mabalozi wa amani kwa kushirikisha jamii nzima katika mijadala na uamuzi unaohusu ustawi wa maeneo yao.
Pia, vijana wanaweza kutumia nafasi zao za uongozi kutoa elimu ya uraia kwa wananchi, hivyo kusaidia kuimarisha mshikamano, uelewano, na ushirikiano miongoni mwa wanajamii.
Vijana mara nyingi huja na mawazo mapya na mbinu za kisasa za kutatua changamoto inayoikabili jamii.
Wanaposhiriki katika kugombea nafasi za uongozi kwenye ngazi za chini kama kijiji na kitongoji, wanaweza kuleta mawazo na mbinu za ubunifu zitakazosaidia kuboresha huduma za kijamii na miundombinu.
Kwa mfano, vijana wanaweza kutumia teknolojia za kisasa kuboresha utoaji wa huduma za afya, elimu, maji na usafi wa mazingira katika maeneo yao.
Aidha, vijana wana uwezo wa kuanzisha miradi mipya yenye tija na inayokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia.
Hii inaweza kujumuisha kuanzisha mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kusimamia rasilimali za kijiji au mtaa, kuanzisha vikundi vya vijana vinavyojikita kwenye biashara na uzalishaji au hata kubuni mikakati mipya ya kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kwenye maeneo yao.
Utawala bora, uwajibikaji
Vijana wakiwa na uongozi kwenye ngazi za chini wanaweza kusaidia kuimarisha misingi ya utawala bora.
Katika nafasi za uongozi kama mwenyekiti wa kijiji, mtaa au kitongoji, vijana wanaweza kusimamia rasilimali za kijiji kwa uwazi na uwajibikaji, hivyo kuzuia mianya ya rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Kwa mfano, vijana wanaweza kutumia ujuzi wao wa kiteknolojia kufuatilia matumizi ya fedha na miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.
Vilevile, vijana wanaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kuonyesha namna bora ya kusimamia maendeleo ya jamii kwa njia za uwazi na ushirikishwaji.
Wanapokuwa kwenye uongozi, vijana wanaweza kujenga mifumo itakayohusisha wananchi wote katika mchakato wa uamuzi, jambo ambalo ni msingi wa utawala bora.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.