Beki wa Yanga, Shomari Kibwana ni kati ya wachezaji ndani wa kikosi hicho ambao mikataba yao inaishia mwisho wa msimu huu (2023/244), lakini bado hajaanza mazungumzo ampya na viongozi wake.
Wakati Yanga ikijivuta kukaa naye mezani, kuna taarifa chini ya kapeti zinaeleza kwamba Azam FC imepeleka ofa ya kuhitaji huduma yake kwa ajili ya msimu ujao.
Tangu Yanga imsajili beki wa kigeni, Kouassi Yao imekuwa ngumu kwa Kibwana kupata nafasi ya kucheza na kuna wakati aliwahi kuandika kwenye ukurasa wake wa instagram kwamba kazini kwake kuna kazi.
Chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, alikuwa anamchezesha Kibwana wakati mwingine beki ya kushoto anayocheza Joyce Lomalisa na Nickson Kibabage, ingawa asilia yake ni beki ya kulia.
Endapo kama Yanga haitamuongezea mkataba, itakuwa imesalia na Yao pekee, lakini pia Kibwana akifanikiwa kusaini Azam FC atakwenda kukumbana na ushindani wa Lusajo Mwaikenda ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango cha juu.
Alipotafutwa Kibwana kuthibitisha juu ya taarifa za kutakiwa na Azam FC, majibu yake yalikuwa haya”Kuna timu nyingi zimeleta ofa, ila mimi bado ni mchezaji wa Yanga na hata ikitokea nikamaliza mkataba, nitawapa nafasi ya kwanza kuwasikiliza waajiri wangu.”
Beki mwingine ambaye Yanga bado hawajakaa naye mezani mkataba wake ukiwa unaishia mwishoni mwa msimu huu ni nahodha Bakari Mwamnyeto.
Msemaji wa Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Zakazi’ aliwahi kusema “Kuna wachezaji kutoka Simba na Yanga ambao mikataba yao,inaishia mwishoni mwa msimu huu.”