Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA), limeeleza matumizi ya vidonge vya P2 sio njia ya uzazi wa mpango, bali hutumika kwa dharura.
Mbali na hilo, imeelezwa moja ya changamoto iliyopo kuhusu elimu ya afya ya uzazi wa mpango ni kutojitosheleza kwa taarifa kuhusu suala hilo, hususani kwa vijana.
Hayo yameelezwa na wadau mbalimbali leo Jumatano Septemba 25, 2024 wakati wakichangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi Space, ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Marie Stopes Tanzania isemayo ‘Uhuru wa Kuamua: Namna upatikanaji wa haki muhimu za afya ya uzazi unavyochangia maendeleo ya Tanzania.’
Kuhusu matumizi ya P2, Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Dk Majaliwa Marwa amesema matumizi ya vidonge vya P2 sio njia ya uzazi wa mpango bali hutumika kama kuna dharura, akitolea mfano wakati ambapo kondomu imepasuka na mhusika yupo siku za hatari anaweza kupewa P2 kama huduma ya dharura.
“Baada ya dharura kupita unarudi kwenye njia yako ya uzazi wa mpango, kwa hiyo sio njia ambayo mtu anaweza kusema hii ndio njia yangu kwa sababu P2 inavyofanya kazi ni kutengeza mazingira mbegu ya mwanaume haitatembea vizuri kufika kwenye yai la mwanamke,” amesema.
Dk Marwa amesema katika matumizi ya P2 watu wengi wamekuwa na mtazamo hasa kuhusisha P2 na utoaji wa mimba jambo ambalo si kweli kwamba kidonge hicho hutumika kuzuia mimba na hutumika ndani ya saa 72 baada ya kujamiiana.
Mbali na hilo amesema haishauriwi kutumia P2 mara kwa mara kwa sababu mtu hujiingiza kwenye dharura nyingi ambazo si nzuri.
Aidha, Dk Marwa amesema sababu ya huduma ya uzazi wa mpango kuwa chini ni elimu.
Amesema watu hawana elimu ya kutosha hasa vijijini kuhusu masuala ya uzazi wa mpango.
“Pia kuna suala la unyanyapaa na hili linahusu hasa vijana na watu ambao hawajaolewa, mtu anahoji unatumia uzazi wa mpango na hujaolewa, kwa hiyo wamefanya uzazi wa mpango ni ya watu walioolewa,” amesema Dk Marwa.
Dk Marwa amesema suala la uzazi wa mpango ni haki ya kila mtu kuamua ni wakati gani apate ujauzito na watoto wapishane kwa umri gani.
Jambo lingine linaloathiri masuala ya uzazi wa mpango ni mila na desturi ambayo huyafanya masuala ya uzazi kuwa na mipaka ya kuzungumzwa ikiwemo mashuleni.
“Hata watoa huduma wakati mwingine na tafiti zimeonyesha hivyo, anapokwenda kijana mdogo kupata habari za uzazi wa mpango ataambiwa muda wako bado, sasa badala ya kupewa taarifa sahihi anaambiwa asubiri hii ndio changamoto,”amesema.
Pia, hoja hiyo ya P2 imezungumzwa na Oscar Kimaro wa Shirika la Marie Stopes Tanzania ambaye amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na mashirika mengine wamefanya utafiti wa matumizi na usambazaji wa dawa za dharura kuzuia mimba P2.
“Utafiti huo umekamilika, Wizara ya Afya na NIMR watatoa matokeo kuonyesha hali ikoje kwa sababu kumekuwepo na mazungumzo mengi mtaani kwamba P2 zimekuwa zikitumiwa kiholela, wanafunzi wanatumia sana, utafiti umeonyesha tatizo sio kubwa sana kwenye hilo kundi ambalo linatajwa na utafiti umefanyika kisayansi,” amesema.
Katika utafiti huo Oscar amesema tatizo halikuwa kubwa kama ambavyo inaelezwa kuwa ni kubwa, hata hivyo watumiaji ni wenye elimu na wanafahamu upatikanaji wa dawa.
Kadhalika, Kimaro amesema baadhi ya watu wenye uwezo wa kufanya uamuzi wa kisera ndani ya nchi ndio wamekuwa wakirudisha nyuma jitihada za utoaji wa elimu ya uzazi wa mpango nchini.
Amesema imani potofu kuhusu uzazi wa mpango umekuwa ukirudisha nyuma jitihada zinazofanywa kufikia malengo ya kitaifa na wanaozisambaza ni watu wenye nafasi kubwa kwenye jamii.
“Wamekuwa na mitazamo inayorudisha jitihada zilizowekwa, ila juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan zinatupa picha kuona tunapoelekea, miaka miwili iliyopita Rais alipokwenda mkoa wa Geita alihusianisha uwezo wa watu na huduma za kijamii na kuwashauri wananchi kuweka breki kidogo,” amesema.
Alidai pamoja na Rais Samia kuunga mkono juhudi hizo bado kuna baadhi ya viongozi waliopo ndani ya Serikali wenye mtazamo hasi kuhusu uzazi wa mpango.
Kimaro amesema katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto ni muhimu jitihada kuwekwa katika utoaji wa elimu ya masuala ya uzazi na huduma zinaenda sambamba na mitazamo, usimamizi ambao ni dira ya Taifa katika maeneo mbalimbali yanayofanyiwa kazi.
Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo, Patrick Kinemo amesema wanatoa huduma za afya ya uzazi kwa kushirikiana na Serikali.
Njia wanazotumia kuwafikia wananchi ni watoa huduma wa shirika hilo kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kuwapatia huduma mbalimbali.
“Wahudumu wanakuwa na ratiba maalumu ya kutembelea vijiji na hii inaratibiwa na Serikali ngazi ya mkoa na wilaya na wananchi wanaelezwa timu itakuwa sehemu fulani, hivyo wanakuja kwenye kituo na kupata huduma na sisi tunaangalia ni maeneo gani ambayo wananchi hawapati fursa hiyo,” amesema.
Kwa upande wa utoaji wa huduma kwa Dar es Salaam na maeneo mengine, Mkurugenzi huyo amesema wana hospitali eneo la Mwenge.
“Katika maeneo mengine mikoani tuna vituo vya afya kwa ajili ya kutoa huduma ya uzazi.”
Amesema utoaji wa huduma katika vituo hivyo ni wananchi kuchangia gharama ndogo.
“Njia nyingine tunawajengea uwezo wahudumu wa Serikali, tayari tuna hospitali 243 ambazo tunafanya nazo kazi kwa ukaribu kuwajengea uwezo wahudumu kwenye vituo kufahamu njia mbalimbali za uzazi wa mpango na kutoa kwa kiwango kinachotakiwa, pia tuna watoa huduma wetu tumewaweka katika vituo hivi kuwajengea wenzao uwezo,” amesema.
‘Vijana wanashiriki tendo kwa kujificha’
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilokuwa na kiserikali la Young & Alive, Sesilia Shirima akichangia mjadala huo amesema moja ya changamoto iliyopo kuhusu elimu ya afya ya uzazi wa mpango ni kutojitosheleza kwa taarifa kuhusu suala hilo, hususani kwa vijana.
Amesema changamoto nyingine ni kutoshirikishwa kwenye programu mbalimbali za afya ya uzazi, sambamba na upatikanaji wa huduma hiyo kwao kutojitosheleza kwa watoa huduma.
Msingi wa kuyasema hayo ni ushiriki wa kundi hilo kwenye tendo la ndoa kwa njia ya kujificha huku wakiwa hawana elimu sahihi ya afya ya uzazi, hivyo wanajikuta wanafanya maamuzi yasiyo sahihi.
Akizungumza kwenye mjadala huo wa Mwananchi Space, Sesilia amesema: “Jamii yetu kwa ujumla inamchukulia kijana ambaye hajafikisha umri wa miaka 18 kama hastahili kushiriki ngono wakati vijana wengi wameshashiriki kwa kujificha, huku wakiwa hawana taarifa sahihi na kunyimwa huduma hivyo wanafanya maamuzi yasiyo sahihi,” amesema.
Amefafanua kijana anapaswa kuwa na elimu kuhusu masuala ya uzazi wa mpango ambayo itamsaidia hata akiingia kwenye ndoa.
Amesema endapo wakipata taarifa na huduma itawarahisishia kwani watafanya maamuzi sahihi.
Amesema vijana wanapaswa kupewa elimu hiyo kwa nguvu kuanzia shuleni kwa kufundishwa ili watilie maanani kama masomo mengine.