BAO pekee la kichwa lililowekwa kimiani dakika ya 13 na beki wa kati, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ jana liliiwezesha Yanga kupata ushindi wa pili mfululizo wa Ligi Kuu Bara na kuchupa kutoka nafasi ya 13 hadi ya saba ikiisogelea Simba ambayo usiku wa leo inashuka uwanjani kucheza na Azam FC.
Huo ni ushindi wa pili wa Yanga ikicheza ugenini, iliupata kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, lakini ukiwa ni wa nane mfululizo kwa timu hiyo katika mashindano yote kwa msimu huu, ikifikisha pia jumla ya mabao 25 huku yenyewe ikiruhusu bao moja tu hadi sasa.
Tofauti na matarajio ya mashabiki wengi wa Yanga waliokuwa wakiamini chama lao lingeweza kutokana na kapu la mabao kutokana na mwendendo mbovu wa KenGold inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, wenyeji hao walicheza kwa nidhamu kubwa na kuwabana watetezi hao, licha ya kutanguliwa kwa bao hilo.
Licha ya kocha Miguel Gamondi kuanzisha kikosi karibu na kile kilichowanyoa CBE SA ya Ethiopia kwa mabao 6-0 katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa wikiendi iliyopita mjini Unguja, Zanzibar akimrudisha kikosini, Khalid Aucho na Dube Abuya na kuwampumzisha Jonas Mkude na Mudathir Yahya, KenGold walionekana kucheza kwa umakini mkubwa kwa muda wote wa mchezo huo.
Kama sio faulo aliyofanyiwa Clement Mzize katika dakika ya 13 na friikiki kupigwa na Stephane Aziz KI kisha Bacca kujitwisha kwa kichwa kuzamisha mpira wavuni mbele ya kipa Castor Mhagama, habari ingekuwa nyingine, kwani licha ya kutengeneza nafasi nyingi, nyota wa Yanga walizipoteza na kuwapa ahueni wenyeji.
Hilo lilikuwa ni la kwanza kwa Bacca msimu huu, lakini ilikuwa ni asisti ya pili kwa Aziz KI msimu huu katika ligi hiyo iliyopo raundi ya tano kwa sasa, huku Yanga ikicheza mechi mbili hadi sasa tofauti na KenGold iliyocheza tano ikiwa haijashinda wala kutoka sare hata moja hadi sasa.
Licha ya Yanga kufunga mabao 6-0 dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mchezo wa jana tatizo la kupoteza nafasi kwa washambuliaji wa Yanga lilionekana kujirudia, huku Mzize akionekana kinara kwa jana mbali Clatous Chama na Aziz Ki.
Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko ya nyota kadhaa hasa eneo la mbele, lakini bado hali iliendelea kuwa ya kosakosa, huku kipa Mhagama akigeuka kuwa shujaa wa KenGold kwa kufanya kazi kubwa ya kuokoa hatari zilizoelekezwa langoni mwake.
KenGold iliyopoteza mechi zote tano ilizocheza hadi sasa na kufungwa jumla ya mabao tisa na yenyewe kufunga mabao mawili yote yakiwekwa kimiani na straika Ibrahim Joshua, ilionekana kuangushwa zaidi na uzoefu mdogo iliyonayo.
Kipa Diarra Djigui aliyekuwa likizo kwa muda mrefu uwanjani, jana alifikisha ‘clean sheet’ ya pili msimu huu katika ya Ligi hiyo, lakini akitimiza dakika 540 ya mechi za mashindano yote, zikiwamo nne za Ligi ya Mabingwa Afrika bila ya kuruhusu bao.
Diarra alifanya kazi ya ziada dakika za lala salama kuokoa mara mbili mipira isiende wavuni baada ya nyota wa KenGold kuitoroka ngome ya Yanga na kupiga mipira iliyokuwa ikionekana ikienda wavuni, ukiwamo mmoja uliogonga nguzo ya kulia kwa kipa na kutambaa na mstari wa goli na kwenda kupita mbele ya nguzo nyingine, huku pia beki wa KenGold, Charles Masai akiokoa mpira wakati ukielekea wavuni baada ya kipa Mhagama kupangua shuti.
Yanga inarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo ujao utakaopigwa wikiendi hii dhidi ya KMC, huku Ken Gold ikisaliwa Sokoine, jijini Mbeya kuipokea Tabora United iliyotoka kufumuliwa mabao 3-1 na Fountain Gate.
Katika mchezo wa mapema uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, jijini Dar es Salaam, JKT ilipata ushindi wa kwanza msimu huu kwa kuichapa Coastal Union 2-1 kwa mabao ya Hassan Dilunga aliyefunga kwa penalti dakika ya 14 na Shiza Kichuya aliyefunga la ushindi dakika ya 48.
Bao la kufutia machozi la Coastal liliwekwa kimiani na Mkenya, John Makwata katika dakika ya 27, ambalo hata hivyo halikuisaidia Coastal kuepuka kipigo cha nne mfululizo katika ligi hiyo.