Dodoma. Mashahidi wawili wa upande wa utetezi wametoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma katika kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 inayosikilizwa faragha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule inawakabili askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Mahakama leo Jumatano Septemba 25, 2024, wakili wa washtakiwa hao, Meshack Ngamando amesema waliotoa ushahidi ni Nyundo na Kindamba. Amesema wawili hao wamekamilisha utetezi wao.
“Kesho tutaendelea kutoa utetezi kwa mashahidi wanane waliobaki maana tuna mashahidi 10 wa utetezi. Muda ukitosha wote watatoa ushahidi wao,” amesema.
Ngamando amesema kesi itaendelea kesho Septemba 26, kuanzia saa 4.00 asubuhi.
Septemba 23, Mahakama iliwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa wote wanne baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake, hivyo kutakiwa kuwasilisha utetezi wao.
Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 18 na vielelezo 12.
Washitakiwa kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Agosti 19, 2024 na kusomewa mashitaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo ambaye mahakamani anajulikana kwa jina la XY.