Dar es Salaam. Imeelezwa ushiriki wa wanaume katika masuala ya uzazi wa mpango ni muhimu na utakuwa na manufaa zaidi ukionekana.
Hayo yamelezwa leo Jumatano, Septemba 25, 2024 na Mkurugenzi wa Shirika Shirika la Marie Stopes Tanzania, Patrick Kinemo katika mjadala wa mtandaoni wa Mwananchi X space.
Mjadala huo umeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Marie Stopes Tanzania ikiwa na mada isemayo: “Namna upatikanaji wa haki muhimu za Afya ya Uzazi unavyochangia maendeleo ya Tanzania’
Kinemo amesema suala la uzazi wa mpango si la wanawake pekee ni la jamii na familia na mwanaume ndiye kiongozi wa familia.
“Ukiangalia katika familia mwanaume ndiyo kiongozi, hivyo maamuzi mengi ya kiuchumi na kiafya ndiye huamua, faida za uzazi wa mpango si za mama na mtoto pekee.
Zipo faida za kiuchumi na ustawi wa familia pale ambapo mama anaweza kutumia njia za uzazi wa mpango na kupata watoto kila baada ya miaka miwili. Ambapo pia inasaidia afya ya mtoto na mama kuimarika,” amesema.
Mbali na hayo, Kinemo amesema uzazi wa mpango humpa mama nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kupunguza mzigo kwenye familia.
“Hivyo ni muhimu wanaume kushiriki kuwashauri akina mama kutumia njia za uzazi wa mpango.”
“Kuna njia za moja kwa moja za kina baba kutumia uzazi wa mpango mfano kondomu na kwa wale waliomaliza majukumu ya kupata watoto wanaweza kufunga njia zao za uzazi,” amesema.
Amesema bado wanaendelea na juhudi za kuwaelimisha akina baba juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango.
Kinemo amesema wanatoa huduma za afya ya uzazi kwa kushirikiana na Serikali.
Njia wanazotumia kuwafikia wananchi ni watoa huduma wa shirika hilo kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kuwapatia huduma mbalimbali.
“Wahudumu wanakuwa na ratiba maalumu ya kutembelea vijiji na hii inaratibiwa na Serikali ngazi ya mkoa na wilaya na wananchi wanaelezwa timu itakuwa sehemu fulani, hivyo wanakuja kwenye kituo na kupata huduma na sisi tunaangalia ni maeneo gani ambayo wananchi hawapati fursa hiyo,” amesema.
Kwa upande wa utoaji wa huduma kwa Dar es Salaam na maeneo mengine, Mkurugenzi huyo amesema wana hospitali eneo la Mwenge.
“Katika maeneo mengine mikoani tuna vituo vya afya kwa ajili ya kutoa huduma ya uzazi.”
Amesema utoaji wa huduma katika vituo hivyo ni wananchi kuchangia gharama ndogo.
“Njia nyingine tunawajengea uwezo wahudumu wa Serikali, tayari tuna hospitali 243 ambazo tunafanya nazo kazi kwa ukaribu kuwajengea uwezo wahudumu kwenye vituo kufahamu njia mbalimbali za uzazi wa mpango na kutoa kwa kiwango kinachotakiwa, pia tuna watoa huduma wetu tumewaweka katika vituo hivi kuwajengea wenzao uwezo,” amesema.
Kwa upande wake, Mtumiaji wa njia ya uzazi wa mpango, Devotha Kihwelo amesema njia ya kalenda imemsaidia kupishanisha watoto wake kwa takriban miaka minane, hali iliyomsaidia kujijenga yeye na familia yake kwa ujumla.
“Nilitumia njia hii kwa kuona ndiyo salama zaidi kwani nilipojaribu kutumia kinga ilinishinda kwa sababu ya kupata muwasho sehemu za siri, hivyo ilinibidi kurudi kwenye njia ya kalenda hadi tulipochukua uamuzi wa kupata mtoto wetu wa pili,” amesimulia.
Devotha ametoa rai kwa wazazi wengine kutumia njia za uzazi wa mpango kwa ajili ya kujijenga wao pamoja na familia zao kama alivyofanya yeye. Amesema baba na mama wanapaswa kukaa kujadili watumie njia gani.
Awali, Mhariri wa Afya wa Mwananchi, Herieth Makwetta akichokoza mada hiyo amesema Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) ya mwaka 2022 unaonyesha asilimia 45 ya wanawake wenye uwezo wa kufanya tendo la ndoa wanaotumia njia za uzazi wa mpango, asilimia 36 wanatumia njia za kisasa na asilimia nane wanatumia za asili.
Hata hivyo, amesema njia ya vipandikizi ndiyo inayotajwa kutumika zaidi miongoni mwa wanawake kwa asilimia 14 ikifuatiwa na njia ya sindano kwa asilimia tisa.
Makwetta amesema takwimu zinaonyesha mwaka 2022 vifo vitokanavyo na uzazi vilikuwa 104 kwa kila vizazi hai 100,000. Hata hivyo, lengo la Serikali ni kupunguza vifo kutoka 104 katika kila vizazi hai 100,000 hadi 70 kufikia mwaka 2025.
“Uzazi wa mpango ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, kwani huokoa maisha kwa kusaidia kupunguza magonjwa ya kina mama na vifo, na kuongeza viwango vya kuishi kwa watoto wachanga,” amesema.
Amefafanua kuwa uzazi wa mpango ni sehemu ya kuboresha afya ya mama na mtoto lakini pia kujenga uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.
Amesema kwamba upatikanaji wa uzazi wa mpango wa hiari na huduma ya afya ya uzazi kwa wanandoa na watu binafsi ni muhimu katika kuhakikisha uzazi salama, familia zenye afya na jamii zinazostawi.