Dar es Salaam. Watu watatu wakiwemo mhasibu na ofisa Tehama wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania (SDA), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka manane, likiwamo la kutakatisha fedha na wizi wa Sh717 milioni mali ya kanisa hilo.
Washitakiwa hao ni ofisa Tehema, Wilson Mapande (35) mhasibu, Winnie Owino (33) na mfanyabiashara, Nicolaus Owino (29).
Watatu hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Septemba 25, 2024 na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga akishirikiana na Wakili wa Serikali, Aaron Titus.
Katuga, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Maximilian Malewo amedai washitakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Kabla ya kuwasomea mashitaka, hakimu Malewo alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Amesema mashitaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washitakiwa hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wanatakiwa kusikiliza mashitaka na hawatatakiwa kujibu chochote.
Akiwasomea mashitaka, wakili Katuga amedai wanakabiliwa na mashitaka manane, la kwanza likiwa ni kuongoza genge la uhalifu, la pili wizi na la tatu hadi la nane ni utakatishaji fedha.
Katika shitaka la kwanza linalowakabili washitakiwa wote, amedai kati ya Mei 2021 na Januari 2023, waliongoza genge la uhalifu kisha kujipatia Sh717.126 milioni kutoka kwenye akaunti ya benki ya CRDB mali ya kanisa hilo.
Shitaka la pili la wizi linamkabili Mapande pekee, anayedaiwa kati ya Mei 2021 na Januari 2023 akiwa mtumishi wa kanisa hilo aliiba Sh717 milioni.
Katika shitaka la tatu la utakatishaji fedha, inadaiwa kwa kipindi hicho Mapande alifungua akaunti benki ya CRDB yenye jina lake akaingiza Sh396.629 milioni.
Shitaka la nne linawakabili Mapande na Winnie wanaodaiwa katika kipindi hicho walifungua akaunti benki ya CRDB yenye jina la Winnie wakaingiza Sh208.468 milioni.
Mbali na hilo, Mapande na Owino wanadaiwa katika shitaka la tano walifungua akaunti benki hiyo na kuingiza Sh112.029 milioni kwa jina la Owino.
Shitaka la sita hadi la nane, linamkabili Mapande na Winnie wanaodaiwa katika kipindi hicho walitumia fedha hizo kununua magari mawili aina ya Toyota Harrier na Toyota Crown. Pia wanadaiwa kununua nyumba eneo ambalo halijapimwa katika Mtaa wa Mtambani, Mapinga, Bagamoyo.
Upande wa mashitaka umedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo umeiomba Mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Malewo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, 2024 kwa ajili ya kutajwa. Washitakiwa wote wamepelekwa rumande.