Chavita wataka kushirikishwa uchaguzi wa serikali za mitaa

Shinyanga. Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) kimeiomba Serikali kuhakikisha wakalimani wa lugha ya alama wanakuwepo kwenye shughuli ya uboreshaji daftari la wapigakura na upigaji wa kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Kwa mujibu wa Chavita, watu wenye ulemavu nchini wanakadiriwa kufikia 5,347,397, kati yao viziwi ni 539,186.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Septemba 25, 2024, na Mwenyekiti wa Chavita nchini, Celina Mlemba katika uzinduzi wa wiki ya viziwi kitaifa uliofanyika ukumbi wa CCM mkoa, mkoani Shinyanga. 

 “Tunaomba Serikali ihakikishe wanakuwepo wakalimani wa lugha ya alama ili kurahisisha utoaji wa taarifa kwa makundi hayo ya watu wenye ulemavu, ikibidi wawasiliane na Chavita ili kupata wakalimani wazuri katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa sababu tumeshuhudia wakati mwingine wanatumika watu wasio na ujuzi wa kutosha kutafsiri mambo,” amesema Mlemba.

Amesema uwepo wa wakalimani wa lugha ya alama katika mchakato huo, siyo tu unaongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maamuzi ya nchi, pia unatoa ajira kwa wataalamu wa kutafsiri lugha ya alama nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chavita Mkoa wa Shinyanga, Frolah Nzelani amewataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha.

“Wazazi wengi wanawaficha watoto wenye ulemavu hasa viziwi wanadhani kuwa baada ya kumaliza hawatapa kazi ya kufanya nawasihi wasiwafiche ndani mnawanyima haki zao za kupata elimu. Hata kwenye uchaguzi ambao wameshafikisha umri wa kupiga kura washirikishwe,”

Akizungumzia changamoto ya mawasiliano wakati wa mchakato wa uchaguzi, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amesema Serikali itatenga bajeti (bila kutaja kiwango) kwa ajili ya wakalimani kuwepo katika kila sekta.

Pia, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu wakiwemo viziwi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, siyo tu kujiandikisha kupigakura bali kuchukua fomu na kugombea katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani.

 “Katika kipindi hiki cha uchaguzi kutakua na wakalimani bobezi Ili kuweka usawa katika utoaji taarifa na nawasihi mjitokeze kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,” amesema Macha.

Mbali na hilo, Macha ameahidi kushirikiana na Chavita ili kuhakikisha hakuna jambo linalokwama ambapo mbali na maadhimisho hayo, kunatarajiwa kufanyika tamasha kesho Septemba 26, 2024 la kumpata miss na mister viziwi mkoani humo.

Related Posts