Kigoma. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Maneno Bufa, mkazi wa Gezaulole ameuawa na watu wasiojulikana, kisha mwili wake ukiwa na majeraha na kutelekezwa eneo la relini, jirani na chanzo cha maji cha Nyakageni, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amekiri kutokea kwa tukio hilo.
“Nipo ziarani, nitakaporejea nitatoa taarifa kuhusu tukio hilo lakini tayari askari polisi wamefika eneo hilo kuuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya taratibu nyingine.”
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa eneo hilo walidai marehemu alikuwa mhalifu wa ubakaji katika maeneo hayo.
Mkazi wa eneo hilo, Masoud Juma alidai shughuli alizokuwa akizifanya marehemu katika mji huo ni za ujambazi, kuteka watu mchana na usiku na kila aliyefika eneo hilo alimtambua kwa kuhusika na tukio la kihalifu kwa namna moja au nyingine.
Naye Iddy Ramdhani amesema hawajashangaa Bufa kuuawa, kwani amekuwa akijihusisha na vitendo vya uhalifu.
“Amekuwa akikamatwa mara kwa mara kwa matukio hayo, lakini baada ya muda tunamuona mitaani akiendeleza uhalifu,”amedai mwananchi huyo.
Kwa upande wake, Amina Salum amesema kuna vijana wengi wanajihusisha na uhalifu katika eneo hilo akiwamo marehemu Bufa, hali inayosababisha wananchi kutokuwa na amani na mali zao pamoja kuhofia usalama wao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwenge, Tatu Kinga amesema mtu huyo amekuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa na matukio ya uhalifu yanayotokea katika mtaa huo na maeneo ya jirani.
Amesema alipokea simu saa 1:30 asubuhi kutoka kwa wananchi kuwa wamekuta mwili wa mtu aliyepigwa na kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali kama panga na wanaomba ushirikiano.
Ameongeza kuwa baada ya kupata simu hiyo kutoka kwa wananchi, aliwasiliana na diwani lakini hakupokea simu, akampigia mtendaji wa kata na kiwenda katika eneo hilo kushuhudia tukio hilo.