Mbinga. Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya kuanza ujenzi wa Bandari ya Mbambabay, wanatarajia kuzungumza na Serikali ya Malawi kuhusu ushirikiano katika huduma za bandari hiyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kufungua milango ya ushirikiano wa kibiashara kupitia bandari hiyo kwa kuwa itahudumia mizigo inayotoka Malawi.
Rais Samia amesema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo unaotarajiwa kufanyika kwa miezi 24, ukigharimu Sh70 bilioni.
Kujengwa kwa bandari hiyo, kunalenga kuimarisha ushoroba wa maendeleo ya Mtwara na kurahisisha uhudumiaji wa mzigo kutoka nchini Malawi kwa kuwa ndiyo njia fupi kutoka Bandari ya Mtwara.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatano Septemba 25, 2024 katika mkutano na wananchi uliofanyika viwanja vya maegesho ya Bandari ya Mbambabay, akiwa katika ziara ya siku sita mkoani Ruvuma.
Amesema uwepo wa bandari hiyo pekee hautatosha kuleta mafanikio yanayotarajiwa, isipokuwa kunahitajika kuwepo huduma nzuri za usafirishaji wa mizigo.
Rais ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia kamati za pamoja, kuzungumza na Serikali ya Malawi.
Mazungumzo hayo amesema yajikite katika kuisihi Serikali ya Taifa hilo ijengwe miundombinu ya kupokea na kusafirisha mizigo kupitia Bandari ya Mbambabay.
“Hii ndiyo diplomasia ya uchumi, nchi moja inaanza lakini mnazungumza na nchi ya pili ili muungane, muelewane na wao waweke miundombinu inayofaa kupokea mizigo itakayotokea Tanzania na hivi ndivyo biashara inavyofanyika,” amesema.
Ushirikiano wa namna hiyo amesema haufanyiki kwenye bandari hiyo pekee, tayari unafanyika katika miradi mbalimbali ukiwamo wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayounganisha Tanzania na Burundi.
Amesema hata barabara kubwa zinazoiunganisha Tanzania, Kenya, Msumbiji na Uganda ni sehemu ya miradi inayotekeleza diplomasia ya uchumi na itifaki za biashara huru katika eneo la Afrika.
Amesema tangu mwaka 2019 akiwa bungeni, amekuwa akimsikia mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya akiomba kujengwa kwa bandari hiyo.
Amesema hatimaye miaka 10 baadaye, ujenzi wa bandari hiyo umeanza kwa kuwekwa jiwe la msingi na kwamba azma hiyo inatimia.
Rais Samia amesema bandari hiyo itarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kutoka na kwenda Malawi na inatarajiwa kuongeza fursa hasa kwa wananchi.
Ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kukamilisha mradi huo kwa wakati, viwango na ubora kama uliokubaliwa katika mikataba.
Akiwa wilayani Nyasa, Rais Samia amezindua Barabara ya Mbinga-Mbambabay yenye urefu wa kilomita 66.
Kuhusu barabara hiyo, amesema ujenzi wake umetokana na ufadhili wa Sh630 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mbali na mradi huo, amesema kwa mara ya kwanza benki hiyo itasaidia mkopo wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) eneo la Kigoma inayounganisha na Taifa la Burundi.
Amewataka madereva wanaotumia barabara hiyo wahakikishe haileti masikitiko kwa ajali, badala yake inawapa furaha.
Awali, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hatua ya kukamilika kwa miundombinu hasa ya Barabara ya Mbinga-Mbambabay inaufungua Mkoa wa Ruvuma ambao awali ulijifunga kwa kushindwa kuingiliana na mikoa mingine.
Amesema Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) imejenga mtandao wa barabara za kiwango cha lami kilomita 12,209 na kati ya hizo, kilomita 2,384 sawa na asilimia 20 ya mtandao wote zimejengwa kwa ufadhili wa Benki ya AfDB.
Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Patricia Laverley amesema kujengwa kwa barabara hiyo ni sehemu ya mchango na ushirikiano wa benki hiyo na Serikali ya Tanzania.
Amesema kukamilika kwake, hakutaishia kupunguza gharama za safari bali hata matengenezo ya magari yanayopita katika barabara hiyo.
“Mwaka jana zaidi ya magari 4,000 yalifanya safari katika barabara hii na kusafirisha abiria na mizigo, lakini mwaka 2015 tulivyokuja ni chini ya magari 150 ndiyo yaliyokuwa yanapita,” amesema Laverley.
Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema barabara hiyo inaunganisha mikoa ya Ruvuma na Mtwara.
“Ujenzi wa barabara hii umefadhiliwa na Benki ya AfDB kupitia mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa Sh670 bilioni na kati ya hizo Serikali imetoa Sh70 bilioni,” amesema.
Besta amesema ujenzi wake umefanywa na kampuni ya uhandisi ya Chico kutoka nchini China na ulikamilika mwaka 2021.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu, Suleiman Kakoso amesema bandari hiyo inaunganisha ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia nchi ya Malawi na itaifanya Bandari ya Dar es Salaam ifanye kazi vizuri.
Amesema zaidi ya kilomita 3,000 za barabara zimejengwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.
“Tunashukuru na tunakuahidi tutaendelea kuiunga mkono Serikali yako,” amesema Kakoso.
Katika mkutano huo, Rais Samia amewataka wavuvi wilayani humo kuhakikisha wanakuwa na vizimba, huku akisisitiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenda kutoa elimu ya uvuvi huo.
Rais Samia ameeleza uvuvi wa vizimba unawapa wavuvi fursa ya kufanya shughuli zao hata Serikali inapofunga maziwa.
“Pale tunapobaini kwamba rasilimali zilizomo ndani ya maziwa zinapungua, huwa tunafunga kwa miezi kadhaa ili rasilimali hizo zijizalishe tena. Kwa hiyo, uvuvi wa vizimba unasaidia msikose kuvua nyakati hizo,” amesema.
Rais Samia amesema pamoja na mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali, kuna changamoto ya makato ya malipo ya wakulima ambayo kwa sasa yanashughulikiwa.
Amewataka wakulima wote, waendelee kuzingatia kanuni za kilimo bora na wavune pale inapokuwa imeiva na hata uzalishaji usiathiri soko la kimataifa.
Kwa kuwa katika eneo hilo wanachimba madini, amesema Serikali itahakikisha inawasaidia wachimbaji hasa wadogo ili wanufaike huku nchi nayo ikinufaika.
Amewataka wachimbaji hao kutouza nje ya nchi madini bila kufuata njia halali, kwa kuwa kufanya hivyo kunaathiri mapato ya Serikali.
Rais Samia ametumia fursa hiyo kueleza kuwa, anatambua uwepo wa baadhi ya vijiji visivyopata umeme, lakini kupitia mradi wa ujazilizi vyote vitapata nishati hiyo.
Uchaguzi Serikali za mitaa
Amesema hana shaka kwamba wilaya hiyo ni ya kijani na njano ingawa ameona rangi nyingine.
Amesema kila mwenye sifa ya kuchaguliwa ahakikishe anaomba nafasi na kwamba, mwenye haki ya kupiga kura ajitokeze kufanya hivyo.
Kuanza Oktoba 11, mwaka huu, amesema wananchi wajitokeze kujiandikisha katika daftari la uboreshaji wa taarifa za mpigakura.
Amesema wananchi wote wanaotaka kuleta fujo kuelekea uchaguzi wanapaswa wakemewe.
“Tusikubali kurudishwa nyuma kwa siasa zisizojali masilahi ya nchi wala sisi wananchi,” amesema.