Dar es Salaam. Wakati Kampuni ya Millicom iliyokuwa ikimiliki chapa ya Tigo, ikidaiwa kufichua taarifa za simu za Tundu Lissu kwa mamlaka za Serikali, Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema) amemtaka wakili wake kuanza taratibu za kisheria ili kubaini wahusika wa shambulio dhidi yake.
Lissu ametoa msimamo huyo akisema: “Tunahitaji kujua na kuambiwa ukweli wote, nani aliyewatuma, vyeo na majina yao, tunataka ukweli wote kutoka kwa Serikali na kutoka kwa Tigo. Tutawashtaki hadi senti ya mwisho. Ukweli huwa haupotei, utacheleweshwa cheleweshwa tu.”
Mwanasiasa huyo amesema hayo leo Jumatano, Septemba 25, 2024 mbele ya waandishi wa habari, makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam, akizungumzia kile kilichoripotiwa na Gazeti la The Guardian la London, nchini Uingereza.
Lissu, ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, alishambuliwa kwa risasi alasiri ya Septemba 7, 2017, nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Gazeti la The Guardian la Uingereza toleo la Jumanne, Septemba 24, 2024, zimedai ushahidi uliowasilishwa Mahakama ya Uingereza na aliyekuwa mchunguzi wa zamani wa kampuni hiyo, Michael Clifford.
Clifford alifutwa kazi na Millicom na baadaye kukimbilia mahakama ya kazi nchini humo.
Jitihada za Mwananchi kuipata Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Tigo Tanzania ambayo imerithi chapa ya Tigo hazijazaa matunda kwani wahusika wametafutwa mara kadhaa bila majibu.
Hata hivyo, Millicom ambayo inatoa huduma zake za mawasiliano kwa masoko ya Amerika ya Kusini na Afrika, imekanusha madai hayo ya Clifford.
Katika utetezi wake, Millicom imedai wakati wanaachana na Clifford walikuwa kwenye mchakato wa kupunguza shughuli zake Afrika hivyo, majukumu ya ofisa huyo yalikuwa na uhitaji kwa wakati huo.
Katika shambulio hilo, Lissu alipigwa kwa risasi akiwa kwenye gari lake na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kushuka ndani ya gari nyumbani kwake Area D akitokea kushiriki kikao cha Bunge.
Baada ya shambulio hilo, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na usiku wa siku hiyohiyo ya Septemba 7, 2024 alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.
Januari 2018, Lissu alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi. Mpaka sasa hakuna aliyekamatwa au aliyehusishwa na shambulio hilo huku Jeshi la Polisi likieleza, uchunguzi unaendelea.
Kwa mujibu wa The Guardian, ushahidi wa Clifford uliowasilishwa mahakamani hapo, unadai Millicom (Tigo) ilidaiwa kuzipa mamlaka za Tanzania taarifa za simu na mahali alikokuwa Lissu kila saa, ndani ya wiki kadhaa kabla ya shambulio hilo.
Clifford anadai Millicom ilimfukuza kazi kutokana na hatua yake ya kuibua wasiwasi kuhusu tukio hilo baada ya kusikia mawasiliano kwenye simu.
“Kesi ya Clifford ni kuwa alitendewa visivyo, akawekwa kando na Millicom na kufukuzwa kazi isivyo haki kwa sababu alitoa taarifa zilizolindwa, au ‘kufichua’ kuhusu masuala muhimu ya usalama wa umma,” wamedai wanasheria wa Clifford katika mawasilisho yao ya maandishi.
Imedaiwa siku tano baada ya Lissu kushambuliwa, Clifford alianza uchunguzi baada ya kusikia sauti kwenye mkutano wa simu kuwa Millicom ilikuwa ikitoa taarifa za simu ya mkononi ya Lissu kwa Serikali ya Tanzania.
Baadaye aliwasilisha muhtasari wa matokeo yake kwa wakuu wake, kulingana na wanasheria wake.
Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa “Taarifa zilitolewa kwa Serikali ya Tanzania tangu Agosti 22, 2017 kupitia mtandao wa WhatsApp,” wanasheria walidai.
“Kuanzia Agosti 29, 2017, kasi ya kumfuatilia Lissu kwa simu iliongezeka na Millicom ilitumia rasilimali zake za kibinadamu na kielektroniki kufuatilia simu mbili za mkononi za Lissu kila saa.”
Hata hivyo, Clifford anadai hakukuwa na ombi rasmi la kisheria la kupokea taarifa hiyo lililofunguliwa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Lissu amesema awali hakuweza kufungua kesi kwa sababu hakuwa na ushahidi wa kutosha, lakini sasa ameupata kupitia kesi hiyo ya Clifford inayoendelea.
“Tumepata pa kuanzia. Tukienda mahakamani tunaiambia Mahakama iwatake walete taarifa ya Clifford. Tulichonacho tunaweza kufungua kesi,” amesema.
Lissu amesema amewasiliana na wakili wake wa kimataifa, Bob Amsterdam kwa kushirikiana na mawakili wenzake kuanza kukusanya ushahidi na mchakato wa kufungua kesi uanze katika mahakama za kimataifa.
“Kesi bado inaendelea huko Uingereza na ndio kwanza imeanza kusikilizwa hadharani, huyu Clifford anaendelea kutoa ushahidi na matumaini yetu ataeleza mambo mengi zaidi, nimemwambia Bob afuatilie na kukusanya nyaraka zote muhimu,” amesema.
“Sasa tukikusanya nyaraka na tukifungua kesi katika mahakama za kimataifa si za hapa kwetu, tunapata mwanya wa kuwajua na waliowawezesha. Tutapata huo ushahidi na tutailazimisha Tigo ituambie ilikuwa inawasiliana na nani, nani wa Serikali aliyeomba.”
Katika msisitizo wake, Lissu amesema: “Kutakuwa na majeshi ya mawakili wa kutosha tena wa kimataifa na tukienda huko walianzishe na nimezungumza na wakili wangu wa kimataifa, Bob Amsterdam, nimemwambia ana mamlaka kamili, Milicon Tigo na dhidi ya Serikali ya Tanzania bila shuruti.”
Lissu amesema katika kesi hiyo hahitaji kupata fedha zitokanazo na gharama za matibabu na fidia: “Tunataka kujua ukweli, nani aliyetoa amri ya niuawe, watuletee ushahidi, wamseme wao, nani aliyewaambia Tigo wanifuatilie, tunataka majina na vyeo na kama Tigo walilipwa, watuambie walilipwa kiasi gani.”
“Tunataka majina ya wahusika wa Tigo na Serikali ya Tanzania na hao walioitwa watu wasiojulikana kwa miaka saba ni kina nani, imani yangu tutawapata na namna ya kuwapata ni kushughulikana nao mahakamani na si Mahakama za Tanzania,” amesema.
Mwanasiasa huyo amesema tangu kushambuliwa kwake kumekuwa na kigugumizi juu ya uchunguzi na mazingira ya eneo alilofikwa na kadhia hiyo inaacha maswali.
Amesema eneo la Area D alilokuwa akiishia linalindwa kwani viongozi mbalimbali wanaishi eneo hilo wakiwemo Naibu Spika wa wakati huo, Dk Tulia Ackson (sasa ni Spika) pamoja na mawaziri mbalimbali.
“Lakini cha kushangaza siku hiyo ya kushambuliwa kwangu, walinzi hawakuwepo, unajiuliza walikwenda wapi, eneo lenye ulinzi hadi wa CCTV kamera kwa nini hazijatumika kuwabaini,” amehoji Lissu na kudai hayo yote yatakwenda kujulikana huko mahakamani.
Lissu amesema kushambuliwa kwake haikumuumiza yeye peke yake: “Bali hata familia yangu, watoto wangu na mke wangu wanatamani kurudi lakini wanasema kile walichokiona Nairobi (jinsi alivyokuwa) hawatamani, nimebaki mimi king’ang’anizi.”
Amesema tukio hilo limemfanya kumwacha na ulemavu wa kudumu ambapo anavaa viatu maalumu huku vyuma na risasi vikiwa ndani ya mwili wake na kusisitiza: “Lazima wote waliohusika tuwajue.”
Aprili 2022, Kampuni ya Millicom International Cellular ilitangaza kukamilisha uuzaji na uhamisho wa shughuli zake nchini Tanzania kwenda kwa kampuni mpya ya Axian kutoka nchini Madagascar (Axian Telecom) ambayo ilirithi mambo yote, yakiwemo madeni.
Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya Axian ndiyo walinunua Kampuni ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo na Zantel) na kwa uhamisho huo, Millicom International Cellular ilipata fedha taslimu Dola za Kimarekani milioni 100 (Sh233 bilioni).
Siku hiyo ambayo Millicom ilitangaza kuuza hisa zake, Axian Telecom ilieleza kwa kushirikiana na Rostam wamekamilisha suala hilo, hivyo kupanua shughuli za kampuni ya Axian ambayo tayari ipo katika mataifa manane ya Afrika.
“Kwa kuitwaa MIC Tanzania plc, Aaxian Telecom inaanza ukurasa mpya Tanzania. Tunayo furaha kuanza safari hii ya kusisimua na wenzetu hapa na tunaamini kwa pamoja tutafanikisha mambo makubwa na kuchangia katika ulimwengu wa kidijitali,” alisema Hassanein Hiridjee, mwenyekiti wa Axian Telecom